Dodoma, 8 Agosti 2026 –
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kutafuta na kufungua masoko ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, hatua inayolenga kuwawezesha wazalishaji kupata masoko ya uhakika na kuongeza tija katika sekta za uzalishaji.
Rais Samia ameyasema hayo leo, Agosti 8, 2026, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wakulima (Nane Nane) Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, Dodoma. Amesema Tanzania imeendelea kufungua milango zaidi kwa biashara na uwekezaji, huku Serikali ikiweka mazingira wezeshi kwa wazalishaji na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Katika kuimarisha uzalishaji wa ndani, Kiwanda cha K4 cha Kilombero Sugar kimetajwa kuwa uwekezaji muhimu katika kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, kupunguza utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi na kuchangia katika safari ya Tanzania kuelekea kujitosheleza kwa sukari.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nane Nane, Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano na Wadau wa Kilombero Sugar, Bw. Victor Byemelwa, amesema kampuni inajivunia uwekezaji wa K4 ambao umeongeza uwezo wa uzalishaji wa sukari na unatarajiwa kuchochea ukuaji wa kilimo cha miwa pamoja na uchumi wa maeneo yanayozunguka shughuli za kampuni.
Amesema uwekezaji huo hauishii katika uzalishaji wa sukari pekee, bali pia una uwezo wa kuongeza uzalishaji wa umeme kutokana na matumizi ya mabaki ya miwa, hatua inayoweza kuchangia katika kuimarisha upatikanaji wa nishati na kuongeza mchango wa kampuni katika gridi ya Taifa.
"Uwekezaji wa K4 ni hatua kubwa katika kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. Pamoja na kuongeza uzalishaji, unafungua fursa nyingi zaidi kwa wakulima wa miwa, ajira, biashara na shughuli nyingine ndani ya mnyororo wa thamani wa kilimo," amesema Byemelwa.
Ametoa wito kwa wananchi, hususan wakulima, kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa kushiriki kikamilifu katika kilimo cha miwa na shughuli mbalimbali zinazohusiana na mnyororo wa thamani, akisema ukuaji wa sekta ya sukari una uwezo wa kuongeza kipato cha kaya na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masuala ya Ushirikiano na Mawasiliano wa Kilombero Sugar, Bw. Derick Stanley, amesema kampuni imejipanga kuongeza uzalishaji wa sukari nchini ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Stanley amesema katika kuongeza uzalishaji wa miwa, Kilombero Sugar inatarajia kushirikiana na wakulima wa nje ya mashamba ya kampuni ambao wanakadiriwa kuzalisha takribani tani milioni 1.5 za miwa, hatua inayotarajiwa kuwawezesha wakulima hao kupata zaidi ya shilingi bilioni 150, hivyo kuongeza kipato cha kaya na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo ya uzalishaji.
"Tunaendelea kuangalia fursa za kuongeza uzalishaji na kujenga uwezo wa muda mrefu wa sekta ya sukari. Uwekezaji huu unalenga si tu kuongeza uzalishaji wa sukari, bali pia kuimarisha mnyororo wa thamani, kuongeza fursa kwa wakulima na kuchangia katika maendeleo ya viwanda nchini," amesema Stanley.
Akizungumzia ushiriki wa Kilombero Sugar katika Maonesho ya Nane Nane jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Biashara wa Kilombero Sugar, Bw. Fimbo Butala, amesema pia kampuni imetumia maonesho hayo kusogeza bidhaa na huduma zake karibu na wananchi, huku ikitoa elimu kuhusu uzalishaji wa sukari, kilimo cha miwa na mchango wa kampuni katika maendeleo ya sekta ya kilimo na viwanda.
Amesema Nane Nane ni jukwaa muhimu la kukutana moja kwa moja na wakulima, wateja na wadau wengine wa sekta ya kilimo, kusikiliza maoni yao na kujenga ushirikiano unaolenga kukuza uzalishaji na kuongeza thamani katika mnyororo wa kilimo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...