Na Mwandishi Wetu, Tanga
SERIKALI imesema mashindano ya ujuzi na ubunifu ni sehemu ya mkakati wa kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwawezesha kushindana katika majukwaa ya kimataifa.

Hayo ameyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, wakati akizungumza katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayoendelea jijini Tanga.

Profesa Nombo amesema Serikali imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuwawezesha vijana kupata ujuzi, ikiwemo kuwatoa darasani na kuwapeleka katika maeneo halisi ya kazi pamoja na kuwashirikisha katika mashindano yanayopima uwezo na umahiri wao.

Amesema Tanzania baada ya kuwa mwanachama wa mashindano ya WorldSkills, imeanza mchakato wa kuwachagua vijana wenye ujuzi kuanzia ngazi za chini hadi mashindano ya kitaifa, ambapo watakaofanya vizuri wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Algeria.

“Tunapotaka kuhamasisha vijana kupata ujuzi, tunatumia mbinu mbalimbali zaidi ya kuwafundisha darasani. Tunataka vijana hawa waende katika maeneo halisi ya kazi ili wapate ujuzi unaotakiwa,” amesema Profesa Nombo.

Amesema vijana wanaoshiriki mashindano hayo wamechaguliwa baada ya kuonyesha umahiri katika fani mbalimbali, huku wataalamu wakifanya tathmini kwa kuzingatia viwango vya kimataifa ili kubaini watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika na baadaye ya dunia.

Profesa Nombo amesema Serikali inalenga kuhakikisha vijana wa Tanzania wanapata fursa ya kuonyesha uwezo wao na kuifanya dunia itambue kuwa nchi ina vijana wenye ujuzi na ubunifu unaoweza kushindanishwa katika majukwaa ya kimataifa.

Amesema Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limeratibu mashindano hayo kwa kushirikisha wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Profesa Nombo, wataalamu wa Wizara ya Elimu na wadau wengine wamepatiwa mafunzo na wataalamu wa kimataifa kuhusu namna mashindano ya WorldSkills yanavyoendeshwa ili kuhakikisha Tanzania inazingatia vigezo vya kimataifa.

Amesema pia viongozi na wataalamu wa Tanzania watashiriki katika kujifunza namna mashindano ya kimataifa yanavyoandaliwa na kuendeshwa, hatua ambayo itasaidia kuboresha zaidi maandalizi ya timu ya taifa.

Profesa Nombo amesema kinachofurahisha katika mashindano hayo ni ushirikiano unaoendelea kati ya taasisi za elimu, vyuo vya ufundi, viwanda na sekta binafsi katika kuwaandaa vijana.

Amesema wataalamu kutoka sekta binafsi na taasisi mbalimbali wamekuwa wakishirikiana na vyuo kutoa maarifa na uzoefu kwa vijana ili kuwawezesha kufanya vizuri katika mashindano hayo.

“Tunakwenda kwenye mashindano haya kama Tanzania iliyounganika kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Lengo ni kuhakikisha tunashiriki kama timu moja ya Tanzania,” amesema.

Amesema ushirikiano huo ni muhimu kwa kuwa unawawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa vitendo na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

Aidha, Profesa Nombo amesema Serikali imeweka mkazo katika elimu jumuishi kwa kuhakikisha vijana wote wanapata fursa ya kutumia vipaji na uwezo wao bila kujali changamoto walizonazo.

Amesema vijana wenye mahitaji maalum wamepewa nafasi ya kushiriki katika mashindano hayo na kuonyesha uwezo wao katika fani mbalimbali.

“Ushiriki wa vijana wenye mahitaji maalum unaonyesha wazi kuwa hata wenye changamoto hizo wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika maisha yao na katika maendeleo ya taifa,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa fursa kwa vijana wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, ili waweze kujenga maisha yao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...