SHIRIKA la uvuvi Tanzania (TAFICO) limeelezea dhamira ya kuwa injini na nyenzo ya kimkakati katika utekelezaji wa Dira 2050, hususani kujenga uchumi wa buluu, kujenga ajira, kuleta mapato ya fedha za kigeni, kukuza viwanda vinavyotegemea rasilimali za maji na kuchochea kasi ya miundombinu ya uvuvi.Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, Dkt. Suleiman Kiula, ndc , leo Agosti 12, 2026, wakati akichangia mada kuhusu “Mapinduzi katika Uvuvi na Ukuzaji Endelevu wa Viumbe Maji katika Kuchochea Utekelezaji wa Dira 2050”, kwenye Kongamano la Uchumi wa Buluu linalofanyika Kizimkazi, Zanzibar.
Dkt. Kiula alikuwa akijibu swali la Muongoza Mada, Prof. Mohammed Sheikh, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), aliyetaka kufahamu namna TAFICO ilivyojipanga katika kutekeleza jukumu lake la kuinua sekta ya uvuvi nchini.
Akijibu, Dkt. Kiula alisema TAFICO ni Shirika lenye uwezo wa kuchochea mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya uvuvi, kuanzia uzalishaji hadi uchakataji na uongezaji thamani.
“TAFICO inakwenda kuwa injini ya Uchumi wa Buluu nchini. Inakwenda kuwa nyenzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya uvuvi nchini,” alisema Dkt. Kiula.
Kauli hiyo inatokana na hatua ambazo TAFICO tayari imeanza kuchukua katika kujenga uwezo wa Taifa katika sekta hiyo, akitaja utekelezaji wa Mradi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko ambao umekamilika, meli moja ya uvuvi wa bahari kuu, huku mchakato wa ununuzi wa meli nyingine nne ukiendelea, mchakato wa ujenzi wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi, kukuza fursa za ajira na biashara pamoja na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Kongamano hilo lenye kauli mbiu “Hifadhi Bahari, Changamkia Fursa za Uchumi wa Buluu” ni sehemu ya shughuli zinazoambatana na Tamasha la Kizimkazi 2026, linalolenga kujadili fursa mbalimbali zinazotokana na Uchumi wa Buluu pamoja na namna ya kuzitumia kwa maendeleo endelevu.
TAFICO inalenga kutumia uwekezaji katika miundombinu, meli za uvuvi na viwanda vya uchakataji kama msingi wa kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya uvuvi na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...