Na Janeth Raphael – MichuziTv
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeweka mkakati wa kuhakikisha kaya zitakazonufaika na Mpango wa Tatu wa TASAF zinatumia fursa zitakazotolewa kujijengea uwezo wa kiuchumi na hatimaye kuondokana na utegemezi ndani ya kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuhitimu kwenye mpango huo.
Mpango huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2026 hadi 2030, ukiwa na lengo la kubadilisha maisha ya kaya maskini kwa kuzipatia fursa za kuongeza kipato, kuimarisha uwezo wa kujitegemea na kujenga msingi wa maendeleo endelevu, badala ya kuendelea kutegemea msaada kwa muda usio na ukomo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shadrack Mziray, amesema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar, iliyotembelea Makao Makuu ya TASAF jijini Dodoma.
Mziray amesema mkakati huo unalenga kuhakikisha kaya zinazonufaika na mpango zinatumia ipasavyo fursa zinazotolewa katika kipindi cha miaka mitatu, kabla ya kuhitimu na kuendelea na maisha ya kujitegemea kiuchumi.
Amesema baada ya kaya kuhitimu, TASAF itaendelea kuzifuatilia ili kutathmini maendeleo yake na kuhakikisha zinabaki katika hali ya kujitegemea kiuchumi.
“Lengo letu ni kuona kaya zinatumia fursa hii kama daraja la kutoka kwenye utegemezi na kujenga uwezo wa kujitegemea. Tunataka wanufaika waweze kuongeza kipato na kuboresha maisha yao kwa njia endelevu,” amesema Mziray.
Kwa upande wa mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo ameishauri TASAF kuendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu, ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa na kaya zinazonufaika zinapata matokeo yaliyokusudiwa.
Wajumbe hao wameeleza kuwa ufuatiliaji wa karibu ni muhimu katika kuhakikisha fursa zinazotolewa kwa kaya maskini zinatumika ipasavyo na kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa wanufaika.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Machano Othman Said, amepongeza TASAF kwa mchango wake katika juhudi za kupunguza umaskini nchini, akisema programu hiyo imeendelea kuwa chachu ya kuwapatia wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar fursa za kuboresha maisha yao.
Machano amesema juhudi za TASAF zimekuwa muhimu katika kuwawezesha wananchi wenye uhitaji kupata fursa zinazowasaidia kuongeza kipato na kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa TASAF unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 650 na unalenga kunufaisha zaidi ya kaya milioni 1.5 zenye uhitaji Tanzania Bara na Zanzibar.
Kupitia mpango huo, TASAF inalenga kuhakikisha uwekezaji unaofanyika kwa kaya maskini hauishii katika kutoa msaada wa muda mfupi, bali unatumika kama msingi wa kuwawezesha wanufaika kuongeza kipato, kujenga uwezo wa kiuchumi na hatimaye kuondokana na utegemezi.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...