Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Jamal Kassim Ali, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Uchumi Tanzania (TISEZA), Ndugu Gilead John Teri, kuhusu fursa za kimkakati za uwekezaji na namna ya kuongeza mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za CCM, Lumumba, Dar es Salaam, yalijikita katika maeneo yenye kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato, ikiwemo uchukuzi na usafirishaji, madini, ardhi na majengo (real estate), pamoja na uwekezaji katika maeneo yenye fursa za kiuchumi.
Pande hizo pia zilijadili namna CCM inavyoweza kuendelea kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kutekeleza kwa ufanisi vipaumbele vilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025–2030, hususan katika kukuza uwekezaji, uzalishaji, ajira na mapato.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndugu Jamal alisisitiza umuhimu wa Chama kuwa na mtazamo wa muda mrefu katika kutambua na kutumia fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Alisema ushirikiano kati ya Chama, taasisi za Serikali, wawekezaji na sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha fursa zilizopo zinabadilishwa kuwa shughuli halisi za kiuchumi zenye tija na manufaa kwa Taifa.
Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi za CCM za kuimarisha ushirikiano na wadau wa uchumi na uwekezaji, kwa lengo la kuongeza ufanisi, mapato na mchango wa rasilimali za Chama katika maendeleo ya Taifa.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...