Na Pamela Mollel, Arusha
Ujerumani kupitia Shirika lake la Maendeleo (GIZ) imeahidi kutoa jumla ya Euro milioni 39.8 kwa ajili ya kuimarisha biashara ya kikanda na ushirikiano wa kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya kukamilika kwa mazungumzo ya ushirikiano wa maendeleo kati ya pande hizo mbili
Akizungumza katika kikao na ujumbe wa Ujerumani, Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen P. Mbundi, ameipongeza Serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuwa mshirika muhimu wa Jumuiya hiyo, akisema mchango wake umekuwa na nafasi kubwa katika kuimarisha mchakato wa ushirikiano na maendeleo ya kikanda
Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayesimamia Masuala ya Forodha, Biashara na Fedha, Annette Ssemuwemba, amesema msaada huo umefika wakati muhimu kwa Jumuiya hiyo ikiwa katika hatua za utekelezaji wa Mkakati wake wa Saba wa Maendeleo, unaolenga kuongeza biashara, uwekezaji na fursa za kiuchumi kwa nchi wanachama
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Afrika Mashariki na Kati katika Wizara ya Shirikisho ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani (BMZ), Joachim Schmitt, Afrika Mashariki ni miongoni mwa maeneo yenye kasi kubwa ya ukuaji wa biashara, hali inayolifanya kuwa eneo lenye mvuto kwa wawekezaji kutoka Ujerumani na Ulaya
Schmitt amesema sehemu ya fedha hizo italenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa biashara ndogo na za kati katika EAC, kupitia ushirikiano wa benki ya maendeleo ya Ujerumani na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki, huku hatua nyingine zikilenga kukuza ushiriki wa sekta binafsi na maendeleo ya mnyororo wa thamani
Aidha, washirika hao wamekubaliana kuendeleza ushirikiano katika maeneo mbalimbali yakiwemo biashara, teknolojia na mabadiliko ya kidijitali, afya, usimamizi wa maji ya mipakani, asasi za kiraia na maendeleo endelevu ya kiuchumi, kwa kushirikisha nchi wanachama, Umoja wa Ulaya, sekta binafsi na washirika wengine wa maendeleo
Katika fedha hizo, Euro milioni 4.8 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha maandalizi na mwitikio dhidi ya mlipuko wa Ebola kupitia mradi wa EAC/GIZ wa Support to Pandemic Preparedness in the EAC Region (PanPrep). Fedha hizo zitatumika katika mafunzo ya wahudumu wa afya, vifaa vya kujikinga, maandalizi ya upatikanaji wa chanjo na dawa, pamoja na uhamasishaji wa jamii kuhusu kinga na chanjo, kwa ushirikiano na Sekretarieti ya EAC, nchi wanachama, Africa CDC na WHO.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...