WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amelielekeza Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kuendelea kusonga mbele katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kubadilisha sekta ya Uvuvi nchini kuwa ya kibiashara, akisisitiza kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali umeweka msingi imara wa kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na rasilimali za uvuvi wa bahari kuu.

Waziri Mkuu ametoa maelekezo hayo leo Agosti 01, 2026, alipotembelea banda la TAFICO katika Maonesho ya Nanenane 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ambapo alipokea maelezo kuhusu shughuli na uwekezaji unaotekelezwa na Shirika kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa.

Akizungumza mara baada ya kupokea maelezo hayo, Mhe. Dkt. Mwigulu alisema Serikali imeonesha kwa vitendo dhamira ya kuibadili sekta ya uvuvi kupitia uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu na vitendea kazi.

"Kupitia uwekezaji huu wa vitendea kazi na miundombinu tunaiona dhamira ya Serikali kwa vitendo katika kuibadilisha sekta hii ya uvuvi iwe ya kibiashara basi niseme tuu Songeni mbele," alisema Waziri Mkuu.

Awali, CPA Matessa alimweleza Waziri Mkuu kuwa Serikali imeendelea kuandika historia katika sekta ya uvuvi kupitia uwekezaji mkubwa utakaoiwezesha TAFICO kupata meli za kisasa za uvuvi wa bahari kuu pamoja na ujenzi wa Bandari ya Uvuvi, ambayo itakuwa kitovu cha shughuli za uvuvi wa bahari kuu nchini.

"Mhe. Waziri Mkuu mpaka sasa Shirika lina meli moja ya uvuvi wa Bahari Kuu na uwepo wa bandari ya uvuvi ambao umekamilika hivi vyote ni vitendea kazi muhimu katika kuleta mapinduzi ya Sekta ya Uvuvi na kuwa ya kibiashara".Alisema CPA.Matessa

Mabadiliko haya ya kisekta yanalenga kuongeza mchango wake katika uzalishaji wa mazao ya uvuvi, uchakataji na kuimarisha mnyororo wa thamani kwa mazao ya uvuvi na kuongeza ajira kwa wanawake na vijana.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na uongozi wa Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)  alipotembelea banda la Shirika hilo katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba  akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa alipotembelea banda la Shirika hilo katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...