Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Ndg. Abdi Mahmoud Abdi, amesema CCM itaendelea kuimarisha uhai na uimara wa chama, ikiwemo kujenga na kuimarisha matawi yake katika majimbo mbalimbali.
Ndg. Abdi ameyasema hayo alipowasili katika Tawi la CCM Kidagoni, Jimbo la Nungwi, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara zake za kukagua na kuimarisha uhai wa CCM kuanzia ngazi ya matawi hadi majimbo.
Amesema uhai na uimara wa chama unategemea kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wanachama wake katika kutekeleza wajibu wao, hususan kulipa ada za uanachama kwa wakati, ambazo huchangia katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama, ikiwemo ujenzi na uimarishaji wa matawi.
Aidha, Ndg. Abdi amesema amezipokea changamoto zilizowasilishwa na viongozi pamoja na wanachama wa Tawi la CCM Kidagoni, zikiwemo ukosefu wa jengo la tawi kwa ajili ya shughuli za chama na changamoto ya miundombinu ya barabara.
Amesisitiza kuwa uongozi wa CCM utaendelea kuzifuatilia changamoto hizo kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji wa chama na kuwawezesha viongozi na wanachama kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Katika ziara hiyo, Ndg. Abdi pia alipata fursa ya kumtembelea na kumjulia hali Ndg. Asiata Hamada Suleiman nyumbani kwake Kidagoni.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...