Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umewahimiza wanafunzi na wahitimu wa Vyuo Vikuu Nchini kuanzisha, kujiunga na kurasimisha vikundi vyao vya ujasiriamali ili kuongeza uwezo wa kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo mikopo, zabuni na huduma nyingine zinazolenga kuwawezesha vijana.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 17, 2026, jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, alipokuwa akitoa wasilisho maalum katika Kongamano la CEO Mindset 2026 lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kufanyika katika Ukumbi wa Confucius Institute wa Chuo hapo.
Kongamano hilo lililenga kuwaandaa wanafunzi na wahitimu wapya kuwa viongozi na wasimamizi wenye uwezo wa kuanzisha na kuendesha taasisi, kampuni na biashara zao kwa ufanisi iliwakutanisha wanafunzi 33 kutoka Ndaki ya Biashara (UDBS), Ndaki ya Elimu (UDSoE), pamoja na Ndaki ya Kilimo na Sayansi ya Chakula (CoAF).
Akizungumza katika kongamano hilo, Bw. Nyaisa alisema urasimishaji wa vikundi ni hatua muhimu kwa vijana wanaotaka kujenga biashara endelevu na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi badala ya vijana kufanya shughuli zao mmoja mmoja, kuunda na kurasimisha vikundi kunaweza kuwawezesha kuwa na nguvu ya pamoja katika kutafuta mitaji, fursa za biashara pamoja na zabuni mbalimbali zinazotolewa na Serikali.
“Vijana mnapaswa kuanza kufikiria zaidi ya mtu mmoja mmoja. Mkiwa katika vikundi vilivyorasimishwa mnaweza kujenga nguvu ya pamoja na kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutafuta fursa za kiuchumi, usajili na urasimishaji wa biashara ni hatua muhimu katika safari ya kijana kutoka kuwa na wazo la biashara hadi kuwa mjasiriamali mwenye shughuli inayotambulika” alisema Bw. Nyaisa
Bw. Nyaisa alisema elimu ya urasimishaji inapaswa kuanza mapema, hususan katika vyuo vikuu, ili wanafunzi waelewe taratibu za kuanzisha na kusimamia biashara kabla ya kuhitimu huku akiwasisitiza walimu na wahadhiri wa masomo ya biashara Chuoni hapo, kutenga muda katika ratiba zao kwa ajili ya kuwaunganisha wanafunzi na wataalamu wa BRELA kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi kupata elimu kuhusu usajili wa kampuni, majina ya biashara na taratibu nyingine za urasimishaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule Kuu ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Prof. Omari Mbura, alimshukuru Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA kwa kutoa elimu kwa wanafunzi waliashiriki Kongamano la CEO Mindset 2026 akisema mchango huo ni sehemu muhimu ya kuwaongezea maarifa yanayohu uongozi, biashara na mazingira halisi ya utendaji baada ya kumaliza masomo. Aliwasisitiza pia wanafunzi kutumia ipasavyo maarifa waliyoyapata na kuendelea kujifunza zaidi.
Nao, baadhi ya wanafunzi waliohudhuria kongamano hilo, walipongeza hatua ya BRELA kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu Bw. Godfrey Nyaisa kwa kushuka hadi ngazi ya vyuo vikuu kutoa elimu hiyo, akibainisha kuwa imewafungua macho kuona jinsi gani mifumo ya kidijitali ya usajili inavyoweza kuwasaidia kuanza safari zao za kiuongozi na kibiashara wakiwa bado masomoni kupitia vikundi vyao.
Ushiriki wa BRELA katika kongamano hilo ni muendelezo wa Wakala kuwafikia vijana katika maeneo mbalimbali na kuwapatia elimu kuhusu usajili wa biashara, urasimishaji na Miliki Ubunifu, hatua ambayo inaendana na mwelekeo wa maendeleo wa Taifa unaosisitiza uwezeshaji wa wananchi kushiriki katika uchumi na kujenga mazingira ya ukuaji wa sekta binafsi. Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo iliridhiwa na Bunge Juni 2025.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...