▪️︎ Atoa rai kwa Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya mafuriko
▪️︎ Aagiza ndani ya Septemba kutangazwa zabuni ya ujenzi wa barabara km 11 za Igauri–Ilongero
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito kwa Watanzania na viongozi katika ngazi zote kuchukua tahadhari na kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño.
Dkt. Mwigulu ametoa rai hiyo leo, Jumapili, Septemba 06, 2026, wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Ilongero, Wilaya ya Singida, mkoani Singida, katika ziara yake ya kikazi ya kusikiliza kero za wananchi na kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema maeneo yenye historia ya mafuriko yanapaswa kutambuliwa mapema na hatua za tahadhari kuchukuliwa, huku akiwataka wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kuzingatia taarifa na maelekezo ya mamlaka husika.
“Maeneo ambayo mnaona ni ya hatari sana Watanzania tunayajua. Tunayajua maeneo yenye historia ya mafuriko. Ni vyema tukaanza kuchukua tahadhari kwa sababu hicho ndicho tunachoweza kukifanya,” alisema.
Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari za mvua, ikiwemo kuwa na magari ya kuchimba mabwawa katika kila ukanda, huku akisisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuepuka kujenga au kuishi katika maeneo yanayofahamika kuwa hatarishi kwa mafuriko.
Kuhusu barabara ya Igauri–Ilongero, Dkt. Mwigulu ametoa agizo la kuhakikisha ndani ya mwezi huu mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa kilomita 11 za awali unakamilika.
“Ndani ya mwezi huu huu, muwe mmeshatangaza kupata mkandarasi wa kuanza kujenga hizi kilomita 11 za awali ambazo zitaziba hili pengo kuanzia hapa mpaka kwenye lami na kupita kidogo mji wa Ilongero,” alisema.
Alisema fedha kwa ajili ya mradi huo zipo na kinachosubiriwa ni kumpata mkandarasi, akisisitiza kuwa ujenzi huo unapaswa kuanza haraka.
Dkt. Mwigulu pia amesisitiza umuhimu wa Serikali kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha zinazookolewa kwenye maeneo yenye kipaumbele, hususan elimu, afya, maji na miundombinu.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza kuanzia mwaka 2028, hivyo Serikali inapaswa kuanza mapema maandalizi ya madarasa, maabara, maktaba na mahitaji mengine ya elimu.
“Ni fedha ya Serikali, ni fedha ya walipa kodi wa Tanzania, ni fedha ambayo inaweza kwenda kutatua hizi changamoto watoto wasikae chini,” alisema.
Kuhusu afya, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ambulensi zinapaswa kuwa tayari muda wote na kuwa na mafuta ili wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na rufaa wasicheleweshwe.
“Ambulensi zetu ziwe standby. Tulishanunua magari, yawe na mafuta. Kila wakati yawe na mafuta. Tusichangishe wagonjwa kuweka mafuta kwenye gari ya Serikali kubeba mgonjwa ambaye yuko mautini,” alisema.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, akisema mfumo huo ni suluhisho la kudumu la kupunguza utegemezi wa michango ya dharura wakati wananchi wanapokabiliwa na gharama za matibabu.
“Watanzania wote tuingie kwenye bima ya afya. Tutaepukana na matatizo mengi sana ambayo tumeyatafutia majawabu ya dharura, lakini yanahitaji yapate majawabu ya kudumu,” alisema.
Kuhusu maji, Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji na umwagiliaji kwa ushirikiano wa wizara zinazohusika, ili miradi hiyo iweze kunufaisha wananchi, mifugo na shughuli za uzalishaji.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia matumizi yenye tija ya rasilimali za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha, ufanisi na mahitaji halisi ya wananchi.





.jpeg)





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...