MKURUGENZI wa Shule ya Green Acres ya Mbezi Beach Salasala, jijini Dar es Salaam, Jackline Rushaigo, amesema shule hiyo imeanza kufundisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ikiwemo akili mnemba, ili kwenda sanjari na ulimwengu wa kidijitali.
Akizungumza kwenye mahafali ya Darasa la Saba na shule ya awali, ambapo wanafunzi 60 walihitimu elimu ya msingi, Rushaigo alisema shule hiyo inatambua umuhimu wa kuzingatia teknolojia za kisasa katika ufundishaji.
“Tumeongeza ubora na ufanisi kwenye TEHAMA, wanafunzi wetu wanajifunza masuala ya akili mnemba wakiwa wadogo hapa shuleni na mambo yanayoendana na uhalisia wa Utanzania wetu na dunia ya sasa,” alisema.
“Tunawapa taaluma ambayo hata wakiwa nje ya shule wanaweza kufanya vitu mbalimbali vya kujiajiri na kujiingizia kipato. Green Acres tunataka mwanafunzi akimaliza hapa awe na ujuzi wa kutosha kabisa kumwezesha kufanya mambo makubwa,” alisema.
Aliwataka wahitimu wa Darasa la Saba kuendelea kuwa na nidhamu, bidii na kujituma katika masomo wanapoingia katika hatua nyingine ya elimu, huku akisema mafanikio ya mwanafunzi hayawezi kutenganishwa na ushirikiano wa karibu kati ya shule, walimu, wazazi na walezi.
Rushaigo aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuiamini Green Acres na kushirikiana na uongozi wa shule katika kuwalea na kuwaandaa watoto wao kwa maisha ya baadaye. Alisema Green Acres itaendelea kuwekeza katika elimu inayolenga kumjenga mwanafunzi kitaaluma, kimalezi na katika nyanja mbalimbali za maisha.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Edwin Odemba, aliwataka wahitimu kuendelea kuthamini elimu, nidhamu na maadili mema wanapoingia katika hatua nyingine ya masomo yao.
Aliwapongeza kwa kumaliza elimu ya msingi na kuwataka kutumia maarifa waliyoyapata shuleni kama msingi wa kujenga maisha yao ya baadaye.
Odemba aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika malezi na elimu ya watoto, akieleza kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanahitaji ushirikiano wa familia, shule na jamii kwa ujumla. Pia aliwapongeza walimu na uongozi wa Green Acres kwa mchango wao katika kuwaandaa wanafunzi kitaaluma na kimalezi.
Aliwataka wahitimu kutambua kuwa kumaliza Darasa la Saba si mwisho wa safari yao, bali ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu inayohitaji kujituma, kujiamini na kuweka malengo ya muda mrefu, huku akiwahimiza kuwa mabalozi wema wa shule yao na kutumia elimu yao kwa manufaa yao, familia zao na jamii.


.jpeg)


.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...