Na Mwandishi Wetu
SHINDANO la kumsaka mrembo wa Kanda ya Mashariki 'Miss Eastern Zone' limezinduliwa kwa kishindo jana usiku Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani.

Akizindua shindano hilo Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir amesema kuwa urembo mashindano ya 'Miss Tanzania'

Kanda ya Mashariki 2026 yana nafasi ya kuwa jukwaa la kukuza vipaji vya wasichana na kuwafungulia fursa za ajira.

Amesema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo uliofanyika Kisemvule Mkoani Pwani pia amewataka wadau na wawekezaji kujitokeza na kutoa udhamini.

DC Khadija amesemakuwa kuwa Serikali kwa kupitia Wilaya hiyo itaendelea kushirikiana na waandaaji kuhakikisha mashindano yanafanyika kwa ufanisi.

Amesema uzinduzi huo ni tukio la kihistoria kwa Mkuranga pamoja na kutoa fursa ya kuitangaza Wilaya hiyo pamoja na fursa zake kwa watu kutoka ndani na nje ya eneo hilo.

“ Uzinduzi huu uliofanyika leo tarehe 18 Septemba 2026 Mkuranga umeandika historia kwa kuweza kuasisi jambo hili kubwa, ambalo linaenda sambamba na sera ya Serikali katika kuhakikisha tunaendelea kukuza sanaa na kuweka mazingira wezeshi kwa sanaa za aina zote kuibua ajira mbalimbali kwa vijana wetu,” amesema.

DC Khadija amewataka wawekezaji na kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano hayo, amesema ushiriki wa sekta binafsi utasaidia kuongeza ukubwa na mafanikio.

Kwa upande wake, Yusuf Hassan, Mkurugenzi wa Miss Tanzania Kanda ya Mashariki, amesema mshindi atazawadiwa gari, huku washindi wa nafasi nyingine wakipata zawadi pamoja na fursa za kuwa mabalozi wa Kampuni na taasisi zitakazoshirikiana na mashindano hayo.

Amesema zawadi hiyo ya gari imetokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali, akiwamo DSTV, Fursa Hub, Kairuki Hospital, Lamata Village na Lamata Foundation.

Aidha, amesema bado wanahitaji wadhamini wakubwa zaidi kwa kuwa bajeti ya mashindano hayo inakadiriwa kufikia takribani Sh Mil. 210, hivyo kuwataka wadau kuendelea kujitokeza.

Yusuf amesema mashindano hayo yatahusisha Mikoa ya Morogoro, Lindi, Mtwara na Pwani, huku warembo 16 watakaofaulu usaili wakitarajiwa kuingia kambini kuanzia Oktoba Mosi kwa ajili ya mafunzo mbalimbali.

Amesema mafunzo hayo yatajikita katika urembo, masuala ya kijamii, uongozi, uchumi na fedha, kabla ya fainali iliyopangwa kufanyika Oktoba 10, 2026.

Miss Tanzania 2022 Halima Kopwe, aliyetokea Kanda ya Mashariki 2022 amesema mashindano ya urembo yamekuwa sehemu muhimu ya safari yake na yalimfungulia fursa mbalimbali baada ya kushiriki shindano la kanda hiyo na baadaye kushinda taji la Miss Tanzania.

Halima, ambaye aliiwakilisha Tanzania katika mashindano ya 'Miss World,', amesema kabla ya kuwa Miss Tanzania alikuwa Miss Mtwara na baadaye kuingia kwenye Kanda ya Mashariki iliyomsaidia kufikia mashindano ya kitaifa.

Naye Hidan Ricco, mwakilishi wa Kamati ya Miss Tanzania iliyo chini ya Lamata Village Entertainment Company Limited, amesema wanafurahishwa kuona mashindano ya kanda yakianza baada ya kuzinduliwa kwa Miss Tanzania wiki iliyopita.

Ricco amesema Kanda hiyo imekuwa kanda ya kwanza kuzindua mashindano yake baada ya uzinduzi wa mashindano ya kitaifa, akisema hatua hiyo inaonesha mwendelezo wa mchakato wa Miss Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...