Na Karama Kenyunko, Michuzi TV

DAR ES SALAAM — Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameiambia Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, kuwa shauri la uhaini linalomkabili ni la kwanza katika historia ya Tanzania ambapo mshtakiwa ni mmoja na shtaka hilo halihusiani na kumuua Rais wala kuipindua Serikali.

Lissu ameyasema hayo wakati akiendelea kutoa majumuisho yake ya mwisho mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Amesema kesi hiyo ni ya tatu ya uhaini katika historia ya Tanzania, akitaja kesi za Grey Likungu Mataka na wenzake ya mwaka 1970 na Khatibu Ghandi na wenzake ya mwaka 1983.

Kwa mujibu wa Lissu, kesi hizo mbili zilizotangulia zilihusu madai ya mipango ya kumuua Rais na kuipindua Serikali kwa kutumia silaha, tofauti na kesi inayomkabili ambayo imefunguliwa chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu, kinachohusu uhaini kwa kuitishia Serikali.

“Tofauti na hizo kesi mbili za mwanzo, hii ya kwangu imefunguliwa chini ya kifungu cha 39(2)(d) na uhaini wa hapa ni wa kuitishia Serikali. Hakuna kumuua Rais wala kuipindua Serikali. Hii ni kesi ya kwanza,” amesema Lissu.

Amesema uamuzi utakaotolewa na Mahakama katika shauri hilo utaweka msingi wa kisheria kuhusu dhana ya uhaini kwa kuitishia Serikali na unaweza kuwa rejea katika kesi zijazo.
“Vyovyote vile mtakavyoamua, mtaweka msingi wa kisheria kuhusu uhaini wa kuitishia Serikali. Waheshimiwa Majaji, mtaweka precedent ambayo itaongoza Mahakama zetu kwa miaka mingi ijayo,” amesema.

Lissu amesema majaji hawataamua tu hatma ya mshtakiwa mmoja, bali pia wataweka msingi wa kisheria utakaoweza kutumika katika kuamua masuala kama hayo kwa miaka ijayo.

“Kwahiyo Majaji, hamtahukumu mtu mmoja, kwahiyo mtaweka utaratibu wa kisheria utakaofuatwa miaka mingi ijayo. Waheshimiwa Majaji wangu, sihitaji kuwakumbusha uzito wa huo mzigo mliobebeshwa. Hamuamui guilt ya mtu mmoja, bali mzigo wa kisheria kwa masuala haya for many years to come,” amesema.

Lissu amesema utetezi wake tangu mwanzo haukuwa wa kukanusha maneno aliyoyasema, bali ulikuwa ukilenga kuieleza Mahakama msingi wa kisheria kwamba, kwa mtazamo wake, kauli za kisiasa hazijawahi kutengeneza kosa la uhaini.

Akiifafanua dhana hiyo ya kisheria, Lissu ametaja hoja sita anazodai zinapaswa kuthibitishwa ili kosa hilo liweze kutengenezwa, ikiwemo kuwepo kwa nia madhubuti (mens rea), uchochezi unaolenga mtu au kundi maalumu la watu, pamoja na matokeo yanayoonekana kwa mujibu wa kifungu cha 10(2) cha Kanuni ya Adhabu.

Amedai kuwa pale sheria inapohitaji kuwepo kwa nia katika kosa, ni lazima matokeo ya nia hiyo yaonekane na kuthibitika. Kwa mtazamo wake, iwapo hakuna matokeo yaliyotokea, maana yake ni kwamba nia hiyo haikutimia na hivyo kosa la uhaini haliwezi kuwepo.

Aidha, Lissu amesema baada ya Mahakama kusikiliza mashahidi 17 wa upande wa mashtaka na kupokea vielelezo 16 vya utetezi, bila kuwepo kwa kielelezo cha Jamhuri, kesi ya Serikali imekuwa dhaifu zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati ilipowasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Katika hatua nyingine ya majumuisho yake, Lissu ameiomba Mahakama kutathmini iwapo yeye ndiye aliyeitisha mkutano huo na kuwaalika wanahabari, pamoja na iwapo alikuwa na nia ya kuchochea kundi la watu kuzuia uchaguzi kwa lengo la kuitishia Serikali.

Kesi hiyo bado inaendelea, huku Lissu akiendelea kuwasilisha majumuisho yake ya mwisho mbele ya Mahakama.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...