Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amezitaka Taasisi za Muungano kuimarisha ushirikiano, kubaini na kutumia fursa zilizopo pamoja na kushiriki kwa pamoja katika shughuli mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuongeza tija na kuleta manufaa zaidi kwa Watanzania.

 Makamu wa Rais ametoa wito huo leo, Septemba 19, 2026 wakati akifungua kikao cha Wakuu wa Taasisi za Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar, na kuhudhuriwa na wakuu wa Taasisi 39 za Muungano.

Makamu wa Rais amewataka viongozi wa taasisi hizo kuelewa kwa kina wajibu wao katika kuwahudumia wananchi na kufanya kazi kwa mtazamo mmoja wa kujenga “nyumba moja”, huku maslahi ya Watanzania yakiwekwa mbele.

Amesema matarajio ya wananchi ni kuona Muungano na taasisi zake zikitoa matokeo yanayogusa maisha yao moja kwa moja, hususan katika kuboresha hali ya uchumi, afya, elimu na maeneo mengine muhimu ya kijamii.

 Amezihimiza taasisi hizo kuondoa vikwazo vinavyoweza kudhoofisha ushirikiano na badala yake kutumia fursa zilizopo katika pande zote mbili za Muungano ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, Mhe. Ndejembi ameahidi kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuunga mkono jitihada za Taasisi za Muungano kwa kuratibu, kusimamia, kushauri na kuziwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.

 Akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema kikao hicho kinalenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Muungano na Ofisi ya Makamu wa Rais; na kuongeza uelewa wa pamoja kuhusu masuala mbalimbali ya Muungano na majukumu yanayotekelezwa na taasisi hizo, sambamba na kuweka mwelekeo wa kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi.

 Kikao hicho cha Wakuu wa Taasisi za Muungano ambacho pia kimehudhiriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mhe Hamza Hassan Juma, Makatibu Wakuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi kinatoa  nafasi kwa viongozi hao kujadili namna ya kuimarisha uratibu, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja itakayoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya wananchi






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...