KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo Taifa, Kenani Kihongosi, amekemea tabia ya baadhi ya wanasiasa kupotosha wananchi kuhusu miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini, akisisitiza kuwa CCM haitavumilia upotoshaji wala matumizi ya uongo katika kuwahadaa Watanzania.

Kihongosi aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Temeke katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Mafuliza, Toangoma, Dar es Salaam.

Alisema ni muhimu wanasiasa kueleza ukweli kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, badala ya kutumia taarifa zisizo sahihi kwa lengo la kupotosha wananchi.

“Lazima tukubaliane, upotoshaji tutaukemea na anayepotosha hatutamvumilia. Tutamwambia, tusitumie uongo kama silaha ya kudanganya Watanzania, tuwaeleze ukweli,” alisema Kihongosi.

Akizungumzia miradi iliyotekelezwa na Serikali, Kihongosi alisema wakati aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, alipofariki, aliacha miradi mbalimbali mikubwa ikiwa inaendelea kutekelezwa, ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR).

Alisema mradi huo umekamilishwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na sasa wananchi wameanza kutumia huduma ya reli hiyo.

“Wakati Dk. Magufuli anafariki aliacha miradi mingi mikubwa. Mradi wa kwanza ulikuwa Reli ya Kisasa (SGR). Leo ile reli imeisha na wananchi wanatumia. Aliyeikamilisha ni Dk. Samia Suluhu Hassan. Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Leo anasimama mtu mmoja na mawazo yake anasema hakuna kilichofanyika,” alisema.

Kihongosi pia alitaja Mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), akisema umekamilika kwa asilimia 100 na tayari umezinduliwa, ukiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme.

Alisema mradi huo umeongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini, huku akitaja pia kukamilika kwa Daraja la Kigongo–Busisi mkoani Mwanza, ambalo sasa linatumika na wananchi.

Kihongosi alisema miradi hiyo ni miongoni mwa ushahidi wa hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha huduma na miundombinu kwa wananchi.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...