Na Sixmund Begashe, Dodoma

Timu za Maliasili Sports Club zimetakiwa kucheza kwa nguvu, juhudi na maarifa katika michezo yote ya Michuano ya SHIMIWI 2026, ili kuhakikisha zinaiwezesha Wizara ya Maliasili na Utalii kupata ushindi wa hali ya juu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Bi. Violeth Mlinga, wakati akiiaga timu hiyo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hassan Abbasi, kabla ya kuanza safari kuelekea Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Bi. Mlinga amesema Wizara imewaamini wanachama wa klabu hiyo, hivyo amewataka wachezaji kuzingatia weledi, nidhamu na taratibu za Utumishi wa Umma ili kulinda taswira ya Wizara na kuhakikisha timu zinaibuka na matokeo chanya.

Amesema ushiriki wa Wizara katika michuano hiyo ni sehemu ya kuendeleza mahusiano mema ya kiutumishi na Wizara nyingine, sambamba na kutumia michezo kutangaza shughuli na majukumu yanayotekelezwa na Wizara kwa maslahi mapana ya taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maliasili Sports Club, Bw. Elia Mtalemwa, amesema klabu hiyo imejiandaa vyema kwa ajili ya michuano hiyo, huku akieleza kuwa lengo kuu ni kurejea na ushindi katika michezo yote.

Ameushukuru uongozi wa Wizara kwa mchango wake katika maandalizi na ushiriki wa klabu hiyo, akisema timu zote zimejiandaa vyema na zimedhamiria kupambana kwa ajili ya ushindi.

Maliasili Sports Club inaelekea Moshi, mkoani Kilimanjaro, kuungana na timu za Wizara nyingine katika Michuano ya SHIMIWI 2026, itakayowakutanisha watumishi kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kushindana katika michezo tofauti.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...