MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeweka lengo la kuongeza thamani ya uwekezaji wake kutoka kiwango cha sasa hadi Tsh trilioni 20.35 ifikapo mwaka wa fedha 2030/31, ikiwa ni ongezeko la asilimia 112.
Akizungumza leo Septemba 21, 2026, jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema lengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa nane unaozingatia nguzo kuu tatu za Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema NSSF itaelekeza mtaji wake kwenye dhamana za Serikali, hatifungani, hisa pamoja na sekta ya viwanda. Alisema Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kilichopo Morogoro kimeleta tija kwa kupata faida ya Tsh bilioni 4.56 katika mwaka 2025/26, huku kikiendelea kuzalisha ajira.
Kwa upande wa kuongeza wanachama alisema NSSF inalenga kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji kutoka milioni 2.1 mwaka 2025/26 hadi milioni 6.6 ifikapo mwaka 2030/31, ikiwa ni ongezeko la asilimia 209. Pia, Mfuko umepanga kutoa ajira zaidi ya 13,000 kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo na uwekezaji.
Katika kuwaingiza waliojiajiri kwenye mfumo rasmi kupitia Skimu ya HIFADHI iliyozinduliwa Februari 2026, NSSF imefanikiwa kuandikisha wanachama 592,791 kutoka sekta isiyo rasmi hadi mwishoni mwa Juni 2026.
Skimu hiyo inalenga wajasiriamali wadogo wakiwamo wakulima, wavuvi, waendesha bodaboda, mamalishe, wachimbaji wadogo wa madini na wamachinga. Mwanachama binafsi anaweza kuchangia Tsh 30,000 kwa mwezi, huku anayehitaji kinga ya kimatibabu kwa familia yake akichangia Tsh 52,200 kwa mwezi.
Kutokana na mwitikio huo, NSSF inalenga kuandikisha wanachama wapya 279,371 kutoka sekta isiyo rasmi katika mwaka wa fedha 2026/27.
Mshomba alisema katika mpango huo wa miaka mitano kuanzia Julai 2026 hadi Julai 2031, NSSF imejikita katika kutekeleza vipaumbele vya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwamo mwongozo wa hifadhi ya mazingira, usawa wa kijamii na utawala bora (ESG) katika shughuli zake za uwekezaji.
Aliwahimiza Watanzania waliojiajiri kuchangamkia fursa ya Skimu ya HIFADHI ili kujenga kesho iliyo salama kiuchumi kwao na familia zao.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, aliipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kurejesha mikutano na wahariri, huku akiahidi ushirikiano na NSSF katika kuelimisha jamii kuhusu miradi inayowagusa wananchi.


.jpeg)
.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...