Na Karama Kenyunko Michuzi tv 

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umefanikiwa kukusanya jumla ya Sh150.04 bilioni kutokana na tozo za matumizi ya Daraja la Nyerere lililopo Kigamboni tangu kuanza kutumika kwake.

Makusanyo hayo yamepatikana katika kipindi cha kuanzia Mei 2016 hadi Juni 2026, kufuatia uzinduzi rasmi wa daraja hilo uliofanyika Aprili 2016.

Akizungumza leo, Septemba 21, 2026, katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, amebainisha kuwa NSSF ilifadhili mradi huo kwa asilimia 100 badala ya asilimia 60 iliyopendekezwa awali.

“Mradi wa ujenzi wa daraja hilo uligharimu shilingi 345.20 bilioni, ambapo bilioni328.74 zilitumika moja kwa moja kwenye ujenzi na shilingi 16.46 bilioni zilitumika kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi.”

Ameeleza kuwa mpango wa uwekezaji uliwekwa kwa muundo wa kimkataba unaoelekeza fedha zote kurejeshwa ndani ya miaka 30 ya uendeshaji kupitia tozo.

Kutokana na mpango huo wa kurejesha uwekezaji ndani ya miaka 30, waendesha vyombo vya moto wanatarajiwa kuendelea kulipa tozo kwa takriban miaka 20 zaidi iliyobaki baada ya miaka 10 ya kwanza ya makusanyo kukamilika.

Amesema, katika kuhakikisha miundombinu hiyo inabaki katika ubora wa hali ya juu na salama kwa watumiaji wote, NSSF imetumia Sh25.81 bilioni kwa ajili ya gharama za uendeshaji, ulinzi pamoja na matengenezo ya mara kwa mara ya daraja hilo.

Aidha, Mshomba amesema kufuatia kuwepo kwa maoni na malalamiko kutoka kwa wananchi wanaoomba viwango vya tozo vipunguzwe zaidi, Serikali imeanza kupitia upya viwango vya tozo zinazolipwa na watumiaji wa daraja hilo.

Mshomba ameeleza kuwa Serikali imeunda timu ya wataalamu inayofanyia kazi suala hilo, na ripoti inatarajiwa kuwasilishwa serikalini hivi karibuni. Mchakato huu unafanyika ingawa viwango vya tozo za kuvuka tayari vilishawahi kushuka huko nyuma.

Timu hiyo inachambua hali halisi ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuamua namna bora ya kuendelea na utaratibu wa tozo pamoja na kurejesha fedha zilizowekezwa. Miongoni mwa njia zinazotazamwa baada ya ripoti kuwasilishwa ni pamoja na uwezekano wa Serikali kuilipa NSSF fedha zilizowekezwa kwenye mradi huo.

Licha ya mchakato huo wa mapitio kuendelea, Mkurugenzi Mkuu alisisitiza kuwa makusanyo ya tozo na shughuli zote za daraja zinaendelea kama kawaida kwa mujibu wa mpango uliowekwa.

Ujenzi wa Daraja la Nyerere umeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kupunguza kero ya msongamano, kurahisisha usafiri kati ya Kigamboni na katikati ya jiji, na kuwa chachu ya ukuaji wa sekta za nyumba, biashara na utalii. NSSF imeahidi kuendelea kulisimamia kwa uwazi ili kulinda maslahi ya wanachama na Mfuko.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...