Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo amemuapisha Mhe. Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, katika hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema maridhiano yaliyofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo ni mwanzo wa hatua mpya katika kuimarisha amani, umoja na utulivu Zanzibar, huku nguvu zikielekezwa katika kuharakisha maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Amesema kuapishwa kwa Othman Masoud ni hatua muhimu katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT Wazalendo, kufuatia Tamko la Pamoja lililotiwa saini Julai 9, 2026 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa maridhiano hayo si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa kazi mpya, akiwataka viongozi na wananchi kuendeleza ushirikiano na kuelekeza nguvu katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na fursa kwa vijana, kuwawezesha wanawake, kuimarisha sekta ya utalii, kuendeleza Uchumi wa Buluu na kuvutia uwekezaji.

Kwa upande wake, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa kumwamini na kumpa dhamana hiyo, akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, weledi na kwa kuzingatia maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.

Uteuzi na kuapishwa kwa Othman Masoud ni sehemu ya utekelezaji wa maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT Wazalendo, yenye lengo la kuimarisha umoja, mshikamano na maendeleo ya Zanzibar.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...