Kampuni ya Sandaland Fashion Wear Limited imetangaza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kauli iliyotolewa hadharani na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhusu jezi za Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Hatua hiyo imetangazwa kupitia tamko rasmi la kampuni hiyo, baada ya kauli ya Makonda iliyotolewa Septemba 16, 2026 kupitia akaunti yake ya Instagram, ambapo alidai kuwa imeathiri jina, chapa, hadhi na uhalali wa bidhaa za Sandaland katika soko.
Katika ujumbe huo, Makonda alinukuliwa akisema:
“Hii sio jezi ya Taifa Stars, Taifa Stars kwa ubora wake hatuwezi kuwa na jezi za kiwango chini hivi. Acheni kutumia picha za Naibu wangu huku ofisi yangu haina taarifa.”
Ujumbe huo uliambatana na picha ya Naibu Waziri Hamis Mwinjuma, maarufu Mwana FA, akiwa amevalia jezi yenye mchanganyiko wa rangi ya njano, bluu, nyeusi na kijani.
Kwa upande wake, Sandaland imesema kauli hiyo imezua taharuki na sintofahamu, huku ikidai kuwa tayari imesababisha madhara ya kiuchumi na kuathiri hadhi ya kampuni.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa ina mkataba halali na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa kutengeneza na kusambaza jezi za Taifa Stars, ambazo zimetumika katika mashindano mbalimbali ya timu za taifa za wanaume na wanawake.
Sandaland imeongeza kuwa haitanyamaza na inakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kauli hiyo, ikidai kuwa ilitolewa kwa namna inayoweza kuchafua chapa yake.
Aidha, kampuni hiyo imesisitiza kuwa imejenga jina na heshima yake kwa muda mrefu na imepewa dhamana ya kushughulikia jezi za Taifa Stars.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...