Na Farida Said Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Mhe. Shaka Hamdu Shaka, leo ameongoza kikao cha Kamati ya Ushauri ya Kodi ya Wilaya kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Kikao hicho kimejadili tathmini ya mwenendo wa makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na kuweka mikakati ya kuimarisha makusanyo kwa mwaka 2026/2027.Akizungumza katika kikao hicho, Shaka amesema kazi ya kukusanya kodi sio ukusanyaji tu, bali ni ujenzi wa maendeleo.
"Sisi sio wakusanya kodi tu, bali ni wajenzi wa maendeleo. Kila shilingi tunayokusanya kwa haki na uadilifu, tunajenga kesho bora ya wananchi wetu. Hivyo jukumu letu sio dogo," alisema Shaka.
Aidha, Shaka ameelekeza kila chanzo cha mapato Wilayani humo kipitiwe upya.
"Kile ambacho kimekufa kifufue, kile ambacho kinalala kiamshwe. Lazima tubadili mtazamo kutoka kudhibiti kwenda kuelimisha umma," alisisitiza.
Ameitaka TRA na Halmashauri kuimarisha matumizi ya takwimu halisi (Data) na kufunga mihuri yote ya uvujaji wa mapato.
"Mapato yanayokusanywa lazima yaingie yote. Tunahitaji uwazi wa mifumo ya ukusanyaji wa kielektroniki. Wilaya ya Kilosa ina uwezo wa kukusanya zaidi ya mara mbili ya tunayokusanya sasa, kama watendaji wataamua kuwa wabunifu na waadilifu," alifafanua.
Shaka amemalizia kwa kusema, "Tusiogope kufanya mapitio magumu. Bora kuwa na vyanzo 20 hai vinavyoingiza kuliko kuwa na vyanzo 100 hewa vinavyotupa sifa bandia."
Naye Katibu wa kikao hicho, Meneja wa TRA Kilosa, Bi. Saada Mtoto, amesema TRA katika kipindi kilichopita imevuka malengo ya ukusanyaji na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa ili kufikia malengo endelevu.



.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...