Na Janeth Raphael - MichuziTv
Serikali imesema ipo katika mashauriano ya kufanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Sheria ya Ndoa kwa lengo la kukabiliana na tatizo la ndoa za utotoni na kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa ya kuendelea na elimu bila vikwazo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema hatua hiyo inalenga kuweka mazingira yatakayowawezesha mabinti kuendelea na masomo kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha sita, huku wakilindwa dhidi ya ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia.
Dkt. Homera ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa programu ya “Sema na Waziri”, ambapo alieleza kuwa Serikali inaendelea na mashauriano kuhusu mabadiliko ya sheria hiyo ili kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto wa kike.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa elimu katika kumwezesha mtoto wa kike kujenga maisha yake na kufikia ndoto zake, akisisitiza kuwa uwekezaji katika elimu na mitaji ni miongoni mwa nguzo muhimu za kuwawezesha wasichana kujikwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amepongeza juhudi zinazofanywa na Plan International Tanzania katika kutetea na kulinda haki za watoto wa kike, akiahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia na kuwawezesha mabinti walio katika mazingira magumu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jane Sembuche, amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 29.1 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kufikisha miaka 18, hali ambayo imekuwa na athari katika fursa zao za elimu na maendeleo ya kiuchumi.
Sembuche ameitaka Serikali kuharakisha mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa ili kuweka miaka 18 kuwa umri wa chini wa ndoa kwa wote, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda haki za watoto na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Dira ya Tanzania 2050.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...