Na Ashura Mohamed, Kilimanjaro

SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuthamini na kuimarisha miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Raymond Mangwala, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Viziwi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Mangwala amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kupitia mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri kwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake, ambapo asilimia mbili hutengwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

“Serikali haitawaacha nyuma watu wenye ulemavu. Tunawahimiza mjitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii ya mikopo. Ni mtaji unaoweza kuwakomboa kiuchumi na kuwawezesha kuanzisha miradi ya kujitegemea,” amesema Mangwala.

Katika hatua nyingine, Mangwala amezitaka taasisi za fedha nchini, ikiwemo Benki ya CRDB, kubuni huduma rafiki na kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa watu wenye ulemavu, hususan viziwi ambao mara nyingi hukumbana na changamoto za mawasiliano.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja Ujumuishi na Fursa Sawa kutoka Benki ya CRDB, Cresensia Grace Kajiru, amesema benki hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa watu wenye ulemavu wa kusikia.

“Kwa kutambua kuwa kila ifikapo Septemba 26 ni Siku ya Viziwi Duniani, sisi kama Benki ya CRDB tunaendelea kuweka mazingira wezeshi, siyo tu kwa kutoa huduma za wakalimani wa lugha ya alama katika matawi yetu yote, bali pia kuwafundisha wafanyakazi wetu kwa vitendo lugha ya alama ili mteja kiziwi akifika ahudumiwe moja kwa moja bila kikwazo,” amesema Kajiru.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) Tawi la Kilimanjaro, Polkarip Josephati Mwacha, akisoma risala kwa mgeni rasmi, amesema licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali, viziwi bado wanakabiliwa na changamoto kubwa katika sekta ya elimu.

Amesema ukosefu wa walimu wenye ujuzi wa kutosha wa lugha ya alama pamoja na vifaa saidizi umechangia viziwi wengi kukosa elimu bora, hali inayowaweka katika mazingira magumu ya kushindana katika soko la ajira na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kisiasa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Tungi Mwanjala, ameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa kuridhia na kusaini Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, ili kulinda na kutetea haki zao kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu vya Watu Wenye Ulemavu, Nassiriya Nassir Ali, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu, huku akiwataka viziwi kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na Serikali ili kujiletea maendeleo.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo Benki ya CRDB, viongozi wa Serikali, taasisi za kifedha, makundi mengine ya watu wenye ulemavu pamoja na wananchi.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...