Benki ya Stanbic Tanzania imesema maboresho ya hivi karibuni katika soko la mitaji nchini yamefungua fursa mpya na muhimu kwa taasisi za umma kupata fedha za muda mrefu kwa ajili ya miradi ya kimkakati.

Benki imetoa kauli hiyo wakati wa Mkutano wa Nne wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum) 2026 ulioanza Jumatatu jijini Arusha.

Zaidi ya wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wakuu 700 wa taasisi za umma wanakutana katika mkutano huo wenye kaulimbiu “Mashirika ya Umma Yenye Ufanisi wa Juu kwa Uchumi Shindani, Shirikishi na Imara katika Kutekeleza Dira 2050.”

Chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania imechukua hatua muhimu mwaka huu katika kuimarisha masoko yake ya fedha. Mwezi Agosti mwaka huu, Benki Kuu ya Tanzania ilitangaza kuwa hati fungani za muda mfupi na hati fungani za Serikali, ambazo tayari zilikuwa wazi kwa wawekezaji wa Kitanzania, sasa zimefunguliwa pia kwa wawekezaji wa kigeni.

Aidha, Serikali imetangaza mipango ya taasisi za umma kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua ambayo itawapa Watanzania fursa ya kumiliki hisa katika taasisi zinazowahudumia.

“Dira 2050 imeweka azma iliyo wazi kwa Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati cha juu na kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Taasisi za umma zina nafasi muhimu katika safari hiyo.” alisema Elias Ngunangwa, Mkuu wa Mahusiano na Wateja Wakubwa, Stanbic Bank.

“Maboresho ya Serikali yanajenga mazingira imara zaidi kwa uwekezaji na mitaji ya muda mrefu. Kama taasisi za kifedha, jukumu letu ni kuleta utaalamu wetu, mitandao yetu na uwezo wetu wa kifedha sambamba na azma hiyo ya Taifa. Tupo tayari kushirikiana na Serikali katika kuitekeleza,” aliongeza.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Stanbic imetoa zaidi ya dola za Marekani bilioni 1 katika ufadhili wa maendeleo nchini Tanzania, ikisaidia miradi ya miundombinu, nishati na biashara.

Euromoney imeitaja Stanbic kuwa Benki Bora ya Uwekezaji Tanzania kwa miaka sita mfululizo, huku Soko la Hisa la Dar es Salaam hapo awali likiitambua kama benki bora ya huduma za uhifadhi wa dhamana.

Ikiwa sehemu ya Standard Bank Group, Stanbic inaunganisha taasisi za Tanzania na mitaji pamoja na utaalamu kutoka Afrika na maeneo mengine duniani.

Stanbic imesema itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Soko la Hisa la Dar es Salaam, pamoja na taasisi za umma, kusaidia hatua inayofuata ya maendeleo ya soko la mitaji.

Benki hiyo ni miongoni mwa wadhamini wa Mkutano wa Mwaka huu, ambao utaendelea hadi Jumatano, 30 Septemba 2026.

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (alieketi) akisalimiana na Mkuu wa Mahusiano ya Wateja Wakubwa, Benki ya Stanbic, Elias Ngunangwa, wakati wa Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026 unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha. Anaeshuhudia ni Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa benki hiyo, Dickson Senzi.














Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...