Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, amekutana na ujumbe wa kampuni ya madini ya AngloGold Ashanti kujadili maendeleo ya shughuli za kampuni hiyo na namna ya kuimarisha uhusiano wake na Tanzania.

Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu, alifanya mazungumzo hayo Jumanne, Septemba 1, 2026, wakati ujumbe wa AngloGold Ashanti ulipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumweleza maendeleo ya shughuli za kampuni hiyo na maslahi yake ya kibiashara nchini Tanzania.

Ujumbe huo uliongozwa na Bi. Lizelle Marwick, Afisa Mkuu wa Sheria wa AngloGold Ashanti, na ulijumuisha Balozi Baso Sangqu, Makamu wa Rais Mwandamizi anayeshughulikia Uendelevu wa AngloGold Ashanti, pamoja na Bw. Simon Shayo, Makamu wa Rais anayeshughulikia Uendelevu na Ushirikishwaji wa wadau wa Geita Gold Mining Limited (GGML).

AngloGold Ashanti ni mojawapo ya kampuni kubwa duniani katika sekta ya madini na inafanya shughuli zake nchini kupitia kampuni tanzu ya GGML.

Akizungumza na ujumbe huo, Bw. Mchechu alisema OTR, kama mwakilishi wa Serikali katika umiliki wa hisa, ni mshirika mwenza wa kampuni hiyo, akisisitiza kuwa mafanikio ya biashara yana manufaa kwa pande zote mbili.

“Nyie msipopata matokeo, na sisi hatupati matokeo; na nyie mkipata matokeo, na sisi tunapata matokeo,” alisema.

Alisema OTR inafanya kazi kwa karibu na mamlaka husika, huku taasisi hizo zikiwa na mtazamo mmoja kuhusu masuala muhimu ili kutengeneza mazingira rafiki zaidi ya uwekezaji.

Bw. Mchechu alisema OTR inalenga kujenga uhusiano wa muda mrefu na AngloGold Ashanti unaozingatia uelewano, utawala bora wa kampuni na mafanikio endelevu ya biashara.

Alisisitiza pia umuhimu wa kuwa na bodi za wakurugenzi zenye watu wenye uwezo, uelewa wa biashara na mtazamo wa kimkakati, akibainisha kuwa wajumbe wa bodi wanapaswa kuwa na uwezo wa kuongeza thamani katika uendeshaji na mwelekeo wa kampuni, hususan katika taasisi zinazochangia kodi na gawio kwa Serikali.

Kwa upande wake, Bi. Marwick alisema AngloGold Ashanti inathamini uhusiano wake na Serikali za nchi ambako inafanya shughuli zake, huku akieleza kuwa kampuni hiyo inatambua umuhimu wa uhusiano wake wa muda mrefu na Serikali ya Tanzania.

Alisema kampuni hiyo inalenga kujenga ushirikiano wa kweli unaowezesha kila upande kutumia uwezo na uzoefu wake katika kutengeneza matokeo yenye manufaa kwa kampuni na nchi kwa ujumla.

Katika kuimarisha uelewa na uwezo wa wajumbe wa bodi, Bi. Marwick alisema AngloGold Ashanti iko tayari kushirikiana katika programu za mafunzo na utangulizi wa majukumu ya bodi, zitakazohusu wajibu wa wajumbe, taratibu za uendeshaji wa bodi na uelewa wa masuala ya fedha.

Pia alipendekeza wajumbe wa bodi kufanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita ili kupata uelewa wa moja kwa moja kuhusu shughuli za uchimbaji, pamoja na masuala ya kitaalamu yanayohusu rasilimali na akiba ya madini.

Alisema uhusiano mzuri uliopo kati ya kampuni hiyo na Serikali unaweza kuwa msingi muhimu wa kuendeleza shughuli zake katika maeneo mengine yenye leseni za utafiti nchini, kwa kuwa kampuni inaweza kupanua shughuli zake kwa urahisi zaidi katika mazingira ambayo tayari ina shughuli, miundombinu na uhusiano mzuri wa kikazi na Serikali.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...