Said Mwishehe,Michuzi TV

TANZANIA kupitia Benki Kuu (BoT) imepata tuzo tano za utambuzi zilitolewa na Jumuiya ya Huduma Jumuishi za Fedha( AFI) ikiwa ni sehemu ya kutambua hatua mbalimbali ilizochukua katika kuimarisha huduma jumuishi za kifedha.

Akizungumza leo Septemba 16,2026 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari kuhusu tuzo hizo Meneja wa Huduma Jumuishi za Kifedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Nangi Massawe amesema AFI ilianzishwa mwaka 2009 .

Ameongeza kuwa AFI ina wanachama kutoka nchi 84 wakati taasisi wanachama zikifikia 90 huku lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata na kutumia huduma rasmi za kifedha kwa usalama na kwa manufaa ya maendeleo yao na uchumi wa nchi.

Ameongeza mkutano wa AFI uliofanyika Septemba mosi hadi 4, mwaka huu nchini Guinea, Tanzania kupitia Benki Kuu imepata tuzo tatu kwa upande wa taasisi na tuzo mbili watu binafsi kutokana na utekelezaji wa mikakati ya huduma jumuishi za kifedha.

Amesema tuzo ya kwanza ni Maya Declaration Award, iliyotolewa kutokana na utekelezaji wa ahadi zilizowekwa na Tanzania, ambapo kati ya ahadi 13, nchi imetekeleza sita ikiwemo kuandaa na kutekeleza mkakati wa Huduma Jumuishi za Kifedha.

“Kwa sasa Tanzania inatekeleza mkakati wa tatu wa huduma jumuishi za kifedha uliowekwa mwaka 2023 na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano hadi mwaka 2028,” amesema Nangi

Pia amesema mafanikio mengine yaliyotambuliwa ni kuongezeka kwa kiwango cha ujumuishi wa kifedha kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka 2023, huku vipimo vya ndani vikionyesha kiwango hicho kimeendelea kukua na kufikia asilimia 80.

Nangi amesema idadi ya watu wazima wasio na huduma za kifedha nayo imepungua kutoka milioni 7.8 mwaka 2017 hadi milioni 6.4 mwaka 2022, wakati upatikanaji wa huduma za kifedha ndani ya umbali wa kilomita tano umeongezeka kutoka asilimia 86 hadi 89.

Pia amesema matumizi ya huduma za fedha kwa njia ya simu yameongezeka kutoka asilimia 60 hadi asilimia 72, huku pengo la huduma za kifedha kati ya wanawake na wanaume likipungua kutoka asilimia 10 mwaka 2017 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022.

“Tanzania pia imeweka mfumo maalumu wa kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha kwa kuhakikisha malalamiko yanafikishwa sehemu sahihi na kufanyiwa kazi, pamoja na kuanzisha programu za elimu ya fedha kwa walio ndani na nje ya mfumo wa shule,”amesema Nangi.

Aidha amesema tuzo nyingine ilitokana na mafanikio ya sera za ujumuishi wa kifedha zinazozingatia wanawake, ikiwemo kuweka kipengele maalumu cha jinsia katika mkakati wa sasa, kubuni bidhaa zinazokidhi mahitaji ya wanawake, kupunguza vikwazo vya upatikanaji wa huduma na kuwezesha wanawake kupata huduma za mikopo na huduma nyingine rasmi za kifedha.

Kuhusu tuzo mbili za mtu binafsi amesema zikitolewa kwa watumishi wa Benki Kuu, akiwemo Dk. Khadija Kishimba na Nangi Massawe kwa kutambuliwa katika maeneo ya uongozi wa kiufundi na sera za huduma jumuishi za kifedha.

Awali Meneja Mifumo ya Malipo ya Taifa kutoka BoT, Mutashobye Mushumbusi ameeleza kuwa benki hiyo imeweka mwongozo wa gharama za huduma za kifedha kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa gharama nafuu.

“Mwongozo huo umeandaliwa kwa kushirikisha watoa huduma za kifedha na tayari umeanza kutumika,unasaidia kupunguza gharama za baadhi ya huduma,”amesema na kusisitiza BoT imeweka mkakati wa kuhakikisha taarifa za gharama za huduma za kifedha zinawekwa wazi kupitia tovuti pamoja na kuwataka watoa huduma kuonesha gharama hizo katika maeneo wanapotoa huduma.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...