Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa salamu za pongezi kwa Baba Mtakatifu Leo XIV, katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, likimtakia afya njema, hekima, nguvu na neema katika kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kichungaji.Katika salamu hizo, TRAMEPRO limemshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha ya Baba Mtakatifu, huku likitambua uongozi wake wa hekima, unyenyekevu na dhamira ya kulitumikia Kanisa.
Shirika hilo pia limeeleza kuthamini ujumbe wa Baba Mtakatifu unaohimiza amani, umoja, huruma, heshima ya utu wa mwanadamu na mshikamano, sambamba na wito wa kulinda mazingira na dunia ambayo imekabidhiwa kwa binadamu.
TRAMEPRO limesema ujumbe huo una umuhimu katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, umasikini na changamoto za afya.
Kwa mujibu wa shirika hilo, afya ya mwanadamu haiwezi kutenganishwa na afya ya mazingira, kwa kuwa maji safi, udongo salama, hewa safi, mimea ya dawa na mazingira bora ni sehemu muhimu ya maisha na ustawi wa jamii.
TRAMEPRO limemtakia Baba Mtakatifu Leo XIV maisha marefu yenye afya njema na utume wenye mafanikio, huku likimuombea aendelee kuwa sauti ya matumaini, amani na upendo kwa watu wote, wanyonge, wagonjwa na wanaohitaji faraja.
Katika salamu hizo, TRAMEPRO limesisitiza kuwa:
“Afya ya mwanadamu na afya ya mazingira ni urithi wa pamoja unaopaswa kulindwa kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.”
Salamu hizo zimetolewa na Boniventura F. Mwalongo, Katibu Mkuu wa Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO).
TRAMEPRO limemalizia kwa kumtakia Baba Mtakatifu Leo XIV baraka na ulinzi wa Mungu, huku likiombea Kanisa, Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...