Na. Vero Ignatus, Michuzi TV – Arusha

​Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za afya ya msingi ili kufikia huduma bora za afya kwa wote huku ikiweka mkazo katika uwekezaji, upatikanaji wa fedha, matumizi ya teknolojia, na kuhakikisha usawa katika utoaji wa huduma hizo nchini.

​Akifunga Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (IPHC2026) kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI Prof. Shemdoe, Naibu Waziri Dkt. Festo Dugange amesema jitihada za Serikali katika kuimarisha afya ya msingi na hospitali za rufaa zimeiwezesha Tanzania kutambulika zaidi barani Afrika.

​Dkt. Dugange ameeleza kuwa hatua hizo kubwa zimesaidia kupunguza vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 mwaka 2015/2016 hadi vifo 104 kwa kila vizazi hai laki moja,Aidha, nchi za Afrika zimehimizwa kujenga mifumo inayostahimili mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza ajenda ya Three Zeros.

​Aliongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya afya lazima uambatane na mnyororo imara wa ugavi wa bidhaa, watumishi wenye ujuzi, dawa, vifaa tiba, na mifumo ya kidijitali. Hatua hii itasaidia taasisi za afya kubadilishana taarifa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

​Mkutano huo umefikia maazimio 10, yakiwemo kuzitaka Serikali za Afrika kuweka afya ya msingi kuwa kipaumbele kwenye bajeti zao. Lengo ni kuongeza fedha za ndani ili wananchi wapate huduma bora, nafuu, na kwa wakati bila kujali maeneo wanayotoka au uwezo wao kiuchumi.

​Pia imesisitizwa kuwa kuimarisha afya ya msingi pamoja na hospitali za mikoa, kanda, na taifa utaongeza uwezo wa mfumo wa afya na kupunguza changamoto za huduma vijijini, ambapo washiriki wanetakiwa kuhakikisha maazimio yote yanatekelezwa kwa vitendo baada ya kurejea makwao.

​Katika hatua nyingine, Dkt. Dugange amesisitiza kila mwananchi apate huduma bila ubaguzi wowote. Ametaka kuimarishwa kwa mifumo ya kidijitali ya taarifa za afya, bima, na ufuatiliaji wa magonjwa ili kuboresha utendaji kazi katika sekta hiyo.

​Maazimio mengine ni pamoja na kuimarisha ufadhili unaozingatia utendaji (performance-based financing), kutekeleza ajenda ya Lusaka, kutumia tafiti kwenye maamuzi, kuendeleza watumishi wa afya, na kuwekeza kwenye malezi ya mtoto kupitia African Union Champion Roadmap on Nurturing Care.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...