Na Janeth Raphael - MichuziTv
Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI), imezitaka taasisi zinazowajibika kuwasilisha taarifa za mapato yatokanayo na rasilimali hizo kwa wakati, ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za Taifa.
Wito huo umetolewa leo Septemba 22, 2026, mkoani Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Balozi Wilson Masilingi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi kutekeleza wajibu wao wa kisheria kwa kuwasilisha taarifa zinazohitajika kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Balozi Masilingi amesema TEITI ina jukumu la kusimamia na kuhakiki taarifa za mapato yanayotokana na shughuli za madini, mafuta na gesi asilia, pamoja na kufuatilia iwapo mapato hayo yanawasilishwa kwa usahihi na hatimaye kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi.
Amesema ushirikiano wa taasisi zinazohusika ni muhimu katika kufanikisha jukumu hilo, hususan kwa kuhakikisha taarifa za mapato na malipo yanayotokana na sekta za rasilimali zinawasilishwa kwa wakati, kwa usahihi na kwa uwazi.
Miongoni mwa taasisi zinazowasilisha taarifa na kuwa chini ya ufuatiliaji wa TEITI ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Taasisi nyingine ni mifuko ya hifadhi ya jamii, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).
Hatua hiyo inalenga kuimarisha mfumo wa uwazi katika sekta za madini, mafuta na gesi asilia, kwa kuwezesha mamlaka husika kupata taarifa sahihi za mapato yanayotokana na rasilimali hizo na kufuatilia namna yanavyokusanywa na kusimamiwa kwa manufaa ya Taifa.



.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...