Vodacom Tanzania Plc leo imezindua ripoti ya Mazingira, Jamii na Utawala (ESG) kwa mwaka uliomalizika Machi 31, 2026, ikionesha kupungua kwa asilimia 24 ya hewa chafu, sambamba na mpango mkubwa zaidi wa uboreshaji wa mtandao katika historia ya kampuni.
Kampuni pia imewekeza shilingi 3.5 bilioni katika ufanisi wa nishati kwa mwaka huu, na kufikisha uokoaji wa megawati 18,340, ikiwa zaidi ya mara sita ya megawati 2,861 zilizookolewa kwa mwaka wa 2025.
Uzalishaji wa hewa chafu ulishuka hadi tani 18,445.5, kutoka tani 24,285.6. Pia, matumizi ya mafuta dizeli yalipungua kwa asilimia 24, kutoka lita milioni 8.6 hadi lita milioni 6.6.
Upunguaji huo ulitokana na kubadilisha vifaa vya zamani vya mawasiliano ya redio katika maeneo 1,808 ndani ya miezi saba, pamoja na uimarishaji wa upatikanaji wa umeme wa gridi uliopunguza muda wa uendeshaji wa jenereta katika vituo vya data vya kampuni.
Mtandao wa Vodacom Tanzania unatumia takriban jigawati (GWh) 169.5 kwa mwaka katika zaidi ya maeneo 3,800, ambapo 2,190 kati yake yapo vijijini. Vituo vya msingi vinachukua asilimia 78.9 ya matumizi yote.
Mwaka huu, maeneo 169 yaliyokuwa nje ya gridi ya taifa yaliunganishwa kwenye gridi ya taifa. Katika kituo cha data cha Kwale, umeme wa gridi ya Taifa uliongezeka kutoka 11kVA hadi 33kVA na kupunguza matumizi ya jenereta kutoka saa 18 kwa siku hadi saa mbili, sawa na upunguzaji wa asilimia 88 wa matumizi ya dizeli katika kituo hicho.
Asilimia 57 ya nishati yote iliyotumiwa na Vodacom Tanzania ilitokana na vyanzo vya nishati jadidifu. Kampuni iliendelea kuhakikisha kuwa umeme wote wa gridi iliyonunua unaendana na nishati inayotokana na vyanzo jadidifu, hatua iliyosaidia kufikia uzalishaji sifuri wa hewa chafuzi. Aidha, Vodacom Tanzania ilihuisha tena cheti chake cha ISO 50001. Uzalishaji wa hewa chafuzi unaotokana na shughuli zake za biashara na mnyororo wake wa thamani pia ulipungua hadi tani 94,944 kutoka tani 100,455.
"Mafanikio haya ya kimazingira yametokana na kufanya uhandisi wa msingi kwa usahihi, siyo kutoka mradi tofauti wa uendelevu," alisema Mkurugenzi wa Miundombinu ya Mtandao Andrew Lupembe huku akiongeza, "kubadilisha vifaa vya zamani katika maeneo 1,808 kunampa mteja muunganisho wa haraka zaidi huku taifa likifaidika na upunguzaji wa athari za mazingira ambazo zingesababishwa na lita milioni mbili zilizopunguzwa kwenye matumizi.”
Wigo wa mtandao wa 4G ulifikia asilimia 76.3 ya wakazi, huku wateja milioni 27.7 wakiwa kwenye mtandao baada ya uzinduzi wa huduma ya kwanza ya 5G nchini Tanzania. Umiliki wa simujanja ulifikia asilimia 46.7, huku wateja 325,415 wakipata vifaa kupitia ubia wa mikopo ya rejareja.
Kwa wateja wasio na simujanja, huduma mpya ya kidijitali inayotumia akili unde inawezesha upatikanaji wa intaneti kupitia jumbefupi (SMS) na simu za sauti, ikisambaza msaada wa kidijitali hadi maeneo ya vijijini.
M-Pesa ilihudumia wateja milioni 14.1 wa ujumuishwaji wa kifedha huku M-Koba, jukwaa la kidijitali la vikundi vya akiba ambao wanachama wake wengi ni wanawake, lilifikia vikundi hai 299,420 huku akiba jumla ikiongezeka kwa asilimia 81.
Vodacom Tanzania Foundation ilifikia wanufaika milioni 2.9, kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania, kampuni iliondoa gharama ya data kwenye jukwaa la kitaifa la maendeleo ya walimu, na kuwapa walimu 121,832 fursa ya kupata nyenzo za maendeleo ya kitaaluma bila gharama ya data. Miti 80,000 ya asili iliongezwa katika Msitu wa Kahe 2 katika Mlima Kilimanjaro.
Kampuni ilirekodi mwaka wa kumi na nne mfululizo bila kutokea kifo cha mfanyakazi mahali pa kazi. Mpango wa uboreshaji ulihusisha wafanyakazi 411 waliosafiri zaidi ya kilomita milioni 1.7, na awamu ya kwanza ilikamilika bila kutokea kifo au tukio kubwa. Vodacom Tanzania ina uthibitisho wa ISO 27001 kwa usalama wa data na haikurekodi faini yoyote ya ushindani usio halali au utakatishaji fedha.
"Nyuma ya kila muunganisho kuna maisha yanayobadilika, mwalimu anayefikia nyenzo za kujifunzia bila gharama ya data, kikundi cha akiba ambacho hakihifadhi tena fedha taslimu katika bati. Tutaendelea kuwajibika kwa wananchi wa Tanzania wanaotuamini kila siku,” aliongeza Philip Besiimire, Afisa Mtendaji mkuu wa kampuni hiyo.
Kwa taarifa zaidi bofya: https://vodacom.com/pdf/our-purpose/reporting-centre/20261/vodacom-tanzania-esg-snapshot-2026.pdf






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...