MRATIBU wa Jukwaa la Kimataifa la Biashara na Uwekezaji la Kilimo na HortiLogistica Africa, Loveness Adolf, amewakaribisha wakulima, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wengine wa sekta ya kilimo kujisajili mapema kushiriki HortiLogistica Africa 2026, itakayofanyika Novemba 8 hadi 10, 2026 katika Hoteli ya Ngurdoto, Arusha.

Amesema jukwaa hilo lenye kaulimbiu “Kuunganisha Masoko, Kukuza Ustawi” linatarajiwa kuwa na zaidi ya waonyeshaji 500 na kuvutia wageni kati ya 10,000 na 12,000, likilenga kuwaunganisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na biashara.

Loveness amesema tukio hilo litatoa nafasi kwa washiriki kuonyesha bidhaa na huduma zao, kujenga mahusiano ya kibiashara na kutafuta fursa mpya katika masoko ya ndani na kimataifa.
Akizungumzia nafasi ya kilimo hai katika uchumi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Bakari Mongo, amesema kilimo hicho kina uwezo wa kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko mbalimbali.

Amesema Tanzania ina fursa kubwa katika uzalishaji wa viungo, mazao ya asili na bidhaa nyingine zinazoweza kuongezewa thamani kupitia uchakataji, hivyo wakulima na wajasiriamali wanapaswa kutumia fursa hizo kukuza biashara zao.

Mongo amesema ushirikiano kati ya wakulima, vikundi vya wazalishaji, wasindikaji, wafanyabiashara na wadau wa uwekezaji ni muhimu katika kuhakikisha bidhaa za kilimo hai zinafikia masoko yenye tija.

Wakati huo huo Loveness amesema Jukwaa hilo litakuwa na shughuli mbalimbali zitakazowapa washiriki nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kufurahia mazingira ya Arusha wakati wa mkutano huo.

Amesema miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni camping, wellness ikiwemo huduma za massage, food fun run kutoka Mbuga kuelekea Arusha National Park, pamoja na programu ya ‘African Invite’ itakayolenga kuonyesha vyakula, utamaduni na burudani mbalimbali za Afrika.

Amesema pia kutakuwa na maonesho yanayoangazia mwelekeo wa sekta ya kilimo na utalii kwa miaka ijayo, yakiwemo maendeleo ya uzalishaji na uuzaji wa mazao kama parachichi, ili kuwawezesha washiriki kupata taswira ya fursa zinazoweza kujitokeza katika sekta hizo.

Kilimo hai chatajwa kuwa fursa ya kukuza biashara na masoko ya kimataifa
Mwanachama wa Taasisi Mwavuli ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Charles Bupamba, amesema wadau wa sekta ya kilimo wanatakiwa kutumia fursa zinazotokana na kilimo hai na kilimo ikolojia kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora, salama na zenye ushindani katika masoko ya ndani na kimataifa. 

Bupamba amesema kilimo hai na kilimo ikolojia si jambo la kupuuzwa, kwani Tanzania ina wakulima na wazalishaji wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwamo viungo, mazao ya asili na bidhaa nyingine ambazo zinaweza kusindikwa, kuongezwa thamani na kuuzwa katika masoko mbalimbali.

Amesema kilimo hai na kilimo ikolojia ni miongoni mwa suluhisho muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo, huku kikitoa fursa kwa wakulima, vikundi vya wazalishaji, wasindikaji, biashara ndogo na za kati pamoja na vijana kuongeza thamani ya mazao na kukuza biashara zao.

Amesisitiza kuwa ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wakulima, wazalishaji na wafanyabiashara, akieleza kuwa majukwaa ya kimataifa yanatoa fursa kwa wadau kuonyesha bidhaa zao, kukutana na wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani, kujenga ushirikiano na wataalamu, kubadilishana uzoefu na maarifa, pamoja na kutafuta masoko mapya. Amesema pia majukwaa hayo yanawezesha wadau kujifunza teknolojia mpya katika kilimo, usindikaji na mifumo ya mnyororo wa thamani, hivyo kuongeza tija na ushindani wa bidhaa za Tanzania.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...