Na Mwandishi Wetu.
Dar es Salaam, Septemba 3, 2026: Wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kupigia kura kazi 294 za uandishi wa habari na makala za maendeleo zilizofuzu katika Samia Kalamu Awards 2026.
Wito huo umetolewa leo, Septemba 3, 2026, na Mwakilishi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa habari (JAB) Prudence Constantine, wakati wa mkutano wa kutangaza kuanza kwa zoezi la upigaji kura litakalodumu hadi Septemba 30, 2026.
Prudence amesema kura za wananchi ni sehemu muhimu ya mchakato wa kumpata mshindi, kwa kuwa zinatoa nafasi kwa jamii kutambua na kuunga mkono kazi zilizoleta mchango au athari chanya katika maisha ya watu na maendeleo ya Taifa.
Amesema wananchi, wakiwa watumiaji wa maudhui ya habari, wana nafasi ya kuchagua kazi wanazoona zimefanya vizuri, zimeakisi mahitaji na maslahi ya jamii na kusaidia kuibua au kuelimisha kuhusu masuala muhimu ya maendeleo.
Wananchi wanaweza kupiga kura kupitia tovuti ya www.samiaawards.tz na kufuata maelekezo yaliyowekwa ili kuchagua kazi wanayoipendelea.
Pia, kura zinaweza kupigwa kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwa kutuma neno “SKA”, likifuatiwa na namba ya mshiriki kwenda 15200.
Akizungumza kuhusu Kazi 294 zilizofuzu kupigiwa kura Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandishi Peter Mwasalyanda amesema kazi hizo zimefuzu baada ya tathmini ya kazi 3,003 zilizowasilishwa na waombaji 985. Jopo la majaji lilifanya tathmini kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na kuteua kazi zilizopata alama za juu.
Naye Mwenyekiti Mwenza wa Mashindano hayo na Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema mashindano hayo yamewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka maeneo ya vijijini na mijini, akisisitiza kuwa washiriki watashindana kwa kuzingatia ubora wa kazi zao na si umaarufu wao.
Kwa mujibu wa mmoja wa majaji wa mashindano hayo, Bi. Beatrice Bandawe, amesema kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopatiwa kipaumbele katika kazi zilizowasilishwa ni pamoja na afya, jinsia na makundi maalum, mazingira pamoja na elimu.
Samia Kalamu Awards zinaandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA kwa Kuhsirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) pamoja na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) zikilenga kutambua, kuenzi na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari na utayarishaji wa makala za maendeleo nchini.





.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...