Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Profesa Peter Msofe, amepongeza Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kwa kuzalisha mbegu bora zenye uwezo wa kustahimili ukame na mvua nyingi, akisema zinaweza kusaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Profesa Msofe ameyasema hayo Oktoba 13, 2026, alipotembelea banda la ASA katika maadhimisho ya kitaifa kuelekea Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga.
Akiwa katika banda hilo, alipata maelezo kuhusu mbegu ya mahindi aina ya T105, inayotajwa kuwa na uwezo wa kustahimili vipindi vya ukame na mvua nyingi, huku ikitarajiwa kutoa mavuno ya magunia 18 hadi 22, kutegemea ukubwa wa eneo na masharti ya uzalishaji.
Afisa Masoko wa ASA, Suzan Ludovick, amesema mbegu hiyo ya uchavushaji huria ina uwezo wa kutoa hadi gunzi mawili kwa kila mmea, hivyo kuwapa wakulima fursa ya kuongeza uzalishaji wanapozingatia kanuni bora za kilimo.
Amesema mbegu hiyo inapatikana kwa wakulima katika maonesho hayo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha matumizi ya mbegu bora zinazoweza kukabiliana na changamoto za hali ya hewa, zikiwemo ukame na mvua nyingi zinazoweza kuathiri uzalishaji wa mazao.
Katika hatua nyingine, Profesa Msofe alipata maelezo kuhusu mbegu ya mpunga aina ya SARO 5, inayoweza kutoa mavuno ya magunia 30 hadi 40 kwa ekari, kutegemea mazingira ya kilimo na usimamizi wa shamba.
Suzan amesema SARO 5 inafaa kwa kilimo cha mpunga katika maeneo ya mabondeni na inakubalika katika soko la mchele kutokana na harufu yake nzuri, sifa inayoweza kuongeza mvuto wa zao hilo kwa walaji.
Ameeleza kuwa matumizi ya mbegu bora zinazolingana na mazingira ya wakulima, yakichanganywa na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo, ni muhimu katika kuongeza tija, kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuboresha kipato cha wakulima.
Juhudi za ASA za kuhamasisha matumizi ya mbegu bora zinatarajiwa kuchangia kuongeza uzalishaji wa mazao, kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na kuimarisha upatikanaji wa chakula nchini.


.jpeg)



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...