Na Janeth Raphael - MichuziTv
Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH) imewataka wadau mbalimbali kuendeleza michango katika mfuko maalumu ulioanzishwa na hospitali hiyo kwa lengo la kugharamia matibabu ya upandikizaji wa uloto na figo kwa wagonjwa wasio na uwezo wa kumudu gharama za huduma hizo.
Wito huo umetolewa wakati wa ziara ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), ikiambatana na wadau wa sekta ya bima, waliotembelea hospitali hiyo kwa ajili ya kujifunza na kujionea huduma za kibingwa zinazotolewa, pamoja na fursa za kushirikiana katika kuboresha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Jesse Kashabano, amesema hospitali hiyo inatoa huduma 18 za kibingwa bobezi na huduma 20 za kibingwa, ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa katika vifaa tiba, teknolojia na wataalamu wenye ujuzi maalumu ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa.
Amesema gharama za upandikizaji wa uloto zinafikia takribani Shilingi milioni 75, huku upandikizaji wa figo ukigharimu karibu Shilingi milioni 45, hali inayowafanya baadhi ya wagonjwa kushindwa kupata matibabu hayo kutokana na changamoto za kifedha.
Dkt. Kashabano amesema gharama hizo ni kubwa hata kwa baadhi ya watumishi wenye kipato, jambo lililoifanya hospitali kuanzisha mfuko endelevu wa kupokea michango kutoka kwa wadau ili kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji.
Ameeleza kuwa mfuko huo ulianzishwa wakati wa maadhimisho ya miaka 10 ya BMH, ukiwa na lengo la kukusanya rasilimali zitakazosaidia kugharamia matibabu ya wagonjwa wanaohitaji upandikizaji wa uloto na figo lakini hawana uwezo wa kulipia huduma hizo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mipango na Fedha wa BMH, Ambele Msika, amesema hospitali ina wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi wote wanaohitaji matibabu, wakiwemo wasio na bima ya afya na wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma wanazohitaji.
Amesema uwepo wa mfuko huo ni hatua muhimu katika kuwezesha hospitali kuwafikia wagonjwa wenye uhitaji, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kuhakikisha changamoto za kifedha haziwi kikwazo cha kupata matibabu.
Naye Naibu Kamishna wa TIRA, Khadija Said, amewaomba wadau wa sekta ya bima na taasisi nyingine kuunga mkono mfuko huo kwa kutoa michango itakayosaidia wagonjwa wanaohitaji huduma za upandikizaji wa uloto na figo.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kusaidia wagonjwa wenye uhitaji na kupanua fursa ya kupata matibabu maalumu ambayo gharama zake ni kubwa kwa wananchi wengi.






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...