Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha
LICHA ya biashara nyingi kuendelea kushamiri nchini Tanzania, bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu umuhimu wa kusajili alama za biashara na huduma, jambo linaloweza kuwaweka wafanyabiashara katika hatari ya kupoteza utambulisho wa bidhaa zao sokoni.
Usajili wa alama za biashara ni miongoni mwa hatua muhimu zinazomsaidia mfanyabiashara kutofautisha bidhaa zake na za wengine, kujenga utambulisho unaotambulika kwa wateja na kulinda maslahi yake katika soko lenye ushindani.
Akizungumzia suala hilo jijini Arusha, Msaidizi wa Msajili Mkuu kutoka Kurugenzi ya Miliki Bunifu ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Nassoro Mtavu, amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya usajili kulinda majina, alama na ubunifu unaotambulisha biashara zao.
Mtavu ameyasema hayo wakati akizungumza na washiriki wa Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni yanayoendelea jijini Arusha , akieleza kuwa BRELA inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa Mtavu, majukumu ya BRELA yanajumuisha usajili wa kampuni za ndani na nje zinazofanya biashara nchini, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, pamoja na uvumbuzi unaohusiana na miliki bunifu.
Amesema huduma hizo zina umuhimu mkubwa kwa wafanyabiashara wanaotaka kuimarisha biashara zao na kuhakikisha utambulisho wa bidhaa zao unalindwa dhidi ya matumizi yanayoweza kuathiri maslahi yao.
"Kwa mfanyabiashara, alama ya biashara si jina au nembo tu, bali ni sehemu ya utambulisho unaowasaidia wateja kuitambua bidhaa yake miongoni mwa bidhaa nyingine zinazopatikana sokoni, " amesema na kuongeza:
"Kwa mfano, wafanyabiashara wanaotengeneza bidhaa za sanaa, mavazi, bidhaa za ngozi na kazi za mikono wanaweza kujenga utambulisho wa biashara zao kupitia majina na alama zinazowatofautisha na washindani wao,".
Amesema ili kulinda utambulisho huo kwa njia ya kisheria, ni muhimu mfanyabiashara kupata taarifa sahihi kuhusu aina ya usajili unaohitajika na taratibu zinazotumika.
Mtavu ameeleza kuwa usajili wa kampuni, jina la biashara, alama ya biashara na uvumbuzi hutegemea mahitaji ya mfanyabiashara, huku akisisitiza kuwa baadhi ya masharti ya uendeshaji wa biashara ni ya lazima kwa mujibu wa sheria.
“Kwenye eneo hili, mfanyabiashara mwenyewe ataamua kusajili ili kulinda kampuni yake, jina la biashara, alama au uvumbuzi wake,” amesema Mtavu.
Ameongeza kuwa mfanyabiashara anaweza kuamua kama anataka kuendesha biashara yake kupitia kampuni iliyosajiliwa au kwa kutumia jina la biashara, kulingana na mahitaji yake.
Mbali na usajili wa kampuni na miliki bunifu, Mtavu amesema BRELA pia inasimamia masuala ya leseni za viwanda na leseni za biashara za kundi A, zinazohusisha biashara zenye wigo wa kitaifa na kimataifa.
Amebainisha kuwa mtu anayetaka kuendesha shughuli za biashara au kiwanda anatakiwa kuzingatia matakwa ya kisheria na kupata leseni inayohitajika kulingana na aina ya shughuli anayoifanya.
Wafanyabiashara wanapaswa kutofautisha kati ya usajili unaolenga kutambua na kulinda biashara zao na vibali vinavyotakiwa kisheria ili kuruhusiwa kuendesha shughuli husika.
Maonyesho ya Kimataifa ya Utalii wa Sanaa na Utamaduni yanayoendelea jijini Arusha yamekuwa jukwaa la kukutanisha wadau wa sanaa, utamaduni na biashara, huku wafanyabiashara wakipata nafasi ya kuonesha bidhaa zao na kujenga mahusiano ya kibiashara.
Kwa wafanyabiashara wanaoshiriki maonyesho hayo, uelewa wa usajili wa alama za biashara na milki bunifu unaweza kuwa hatua muhimu katika kukuza biashara zao na kuongeza uwezo wa bidhaa za Kitanzania kushindana sokoni.
Ujumbe wa BRELA kwa wafanyabiashara ni kwamba, pamoja na kuzalisha bidhaa bora na kutafuta masoko, ni muhimu pia kufahamu taratibu za kusajili na kulinda utambulisho wa biashara zao ili kuimarisha misingi ya ukuaji endelevu wa biashara nchini.

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...