Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

SPIKA wa Bunge la Australia, Milton Dick, amechaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) baada ya kupata kura 182 sawa na asilimia 56 ya kura zote 

Akitangaza matokeo ya washindi, Rais anayemaliza muda wake Dkt Tulia Ackson amesema nafasi ya pili ilichukuliwa na Spika wa Azbeijan  Ms.Sahiba Gafarova  aliyepata kura 124 sawa na asilimia 38 na mgombea wa mwisho ni Spika wa Bunge la Chile Rojo Edward Silver aliyepata kura 21 sawa na asilimia 6.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Milton Dick, ameahidi kuimarisha demokrasia, amani na ushirikiano wa kimataifa, akiwashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo kwa kumwamini na kumpa dhamana ya kuongoza taasisi hiyo.

Amesema anapokea jukumu hilo kwa unyenyekevu na kutambua wajibu mkubwa aliopewa wa kuhakikisha kila taifa, bila kujali ukubwa wake, utajiri au ushawishi wake, linaheshimiwa na kupata nafasi ya kusikilizwa katika jukwaa la kimataifa.

"kuchaguliwa kwangu ni ukumbusho kwamba demokrasia, kuheshimiana na ushirikiano bado ni misingi muhimu katika kuunganisha mataifa na kutafuta majibu ya changamoto zinazolikabili dunia," amesema.

Dick amesema atafanya kazi kwa karibu na wajumbe wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali ili kujenga mazingira ya mazungumzo, kuimarisha uelewano na kutafuta maeneo ya kukubaliana licha ya tofauti za kisiasa, tamaduni, lugha na imani.

Amesisitiza kuwa changamoto za dunia, ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, haziwezi kutatuliwa na taifa moja au eneo moja pekee, hivyo zinahitaji ushirikiano wa pamoja, akitaja umuhimu wa kuzingatia mazingira magumu yanayokabili mataifa ya visiwa vya Pasifiki na nchi ndogo.

Amesema katika uongozi wake atahakikisha kuwa sauti za mataifa yote zinasikilizwa na maslahi yake yanazingatiwa, akieleza kuwa hakuna nchi inayopaswa kutengwa katika mijadala ya kimataifa kwa sababu ya ukubwa wake, utajiri au nafasi yake ya kijiografia.

Katika hatua nyingine, Dick ametangaza mpango wa utekelezaji wa siku 100 za kwanza za uongozi wake, akieleza kuwa ataanza mara moja kufanyia kazi vipaumbele vilivyowekwa kwa ajili ya kuimarisha utendaji na malengo ya taasisi hiyo.

Amesema IPU ilianzishwa kwa maono ya kujenga taasisi inayotumia mazungumzo kutatua tofauti badala ya kuendeleza migawanyiko, huku ikitetea demokrasia na kuhimiza amani katika mataifa mbalimbali duniani.

Ameahidi kuongoza kwa unyenyekevu, uadilifu na heshima, akisisitiza kuwa atakuwa tayari kusikiliza maoni ya wajumbe na kuweka mbele maslahi ya IPU pamoja na wananchi wanaowakilishwa na mabunge yao.

Dick amesema mabunge yana wajibu mkubwa katika kipindi hiki cha changamoto na kutokuwa na uhakika duniani, kwa kuwa wananchi wanategemea viongozi wao kulinda demokrasia, kuimarisha amani, kutetea uhuru na kujenga mazingira bora kwa familia na watoto.

Ameongeza kuwa jukumu la kuendeleza misingi hiyo si la kiongozi mmoja pekee, bali ni wajibu wa pamoja wa wabunge na viongozi kutoka mataifa yote yanayoshiriki katika IPU.

Amesema anaamini kuwa mambo yanayoyaunganisha mataifa ni makubwa kuliko tofauti zinazoweza kuyatenganisha, hivyo amewataka wajumbe kuendelea kushirikiana katika kujenga mustakabali wenye amani, usalama na maendeleo.

Katika kuhitimisha hotuba yake, Dick ameomba mwongozo na hekima katika kutekeleza majukumu yake mapya, akieleza dhamira yake ya kutumia nafasi hiyo kujenga madaraja ya ushirikiano na kuimarisha demokrasia kwa manufaa ya watu wote duniani.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...