.jpeg)
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
NCHI nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika zimetakiwa kuimarisha ufadhili, udhibiti wa mafuriko na uhifadhi wa samaki ili kulinda ziwa hilo na jamii zinazotegemea rasilimali zake kwa maisha na shughuli za kiuchumi.
Mwenyekiti wa kikao cha maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), Dkt. Douty Chibamba, ametoa wito huo leo Oktoba 29, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maandalizi ya Mkutano wa 14 wa Kawaida wa Mawaziri wa mamlaka hiyo.
Dkt. Chibamba amesema upatikanaji wa fedha za kutosha na za uhakika, pamoja na maamuzi yanayozingatia ushahidi wa kisayansi, ni muhimu katika kutekeleza makubaliano ya kikanda na kufikia malengo yaliyowekwa.
Amewataka wajumbe kuandaa mapendekezo mahususi kuhusu mpango kazi na bajeti ya mwaka 2027, akisisitiza kuwa Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania na Zambia zinapaswa kuhakikisha vipaumbele vyao vinaendana na upatikanaji wa fedha na watumishi wenye sifa stahiki.
“Vipaumbele vyetu lazima viambatane na ufadhili wa kutosha na wa uhakika, ikiwemo kutimiza kwa wakati wajibu wa kifedha wa nchi wanachama,” amesema.
Akizungumzia udhibiti wa mafuriko, Dkt. Chibamba ametaja pendekezo la kuondoa tope na mchanga katika Mto Luga na kufanya upembuzi yakinifu kuhusu uwezekano wa kujenga bwawa la kudhibiti viwango vya maji katika Ziwa Tanganyika.
Amesema mapendekezo hayo yanahitaji tathmini za kina za kisayansi na kiufundi ili kubaini uwezekano wa kuyatekeleza na athari zake kwa jamii, miundombinu na mazingira.
Kuhusu uvuvi, amehimiza kufanyika kwa tafiti za kisayansi zitakazobaini hali ya akiba ya samaki na kusaidia kuweka mikakati ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.
Aidha, amewataka wajumbe kuchambua ripoti ya mwaka ya mamlaka hiyo, kubaini mapungufu ya kiutendaji na kupendekeza hatua za kuimarisha uwajibikaji, uratibu na utendaji, huku nchi wanachama zikishughulikia changamoto za uhaba wa fedha na watumishi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Reuben Kwagilwa, amesema ushirikiano wa Burundi, DRC, Tanzania na Zambia ni muhimu katika kusimamia rasilimali za ziwa na kulinda mazingira kwa manufaa ya jamii zinazozitegemea.
Amesema wajumbe wanatarajiwa kuwasilisha mapendekezo kuhusu sera, masuala ya kiufundi, uimarishaji wa taasisi na ufadhili ili yazingatiwe na mawaziri katika mkutano huo.
Mkutano huo umewakutanisha maafisa wa serikali, wataalamu na washirika wa maendeleo kutoka nchi hizo nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika.




.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...