Na Victor Masangu, Pwani

Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Pwani kimeiomba Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa huo kuwahimiza waajiri kutekeleza wajibu wao wa kufanya vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kwa mujibu wa taratibu na matakwa ya kikatiba.

Ombi hilo limetolewa na Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susan Shesha, Oktoba 10, 2026, wakati wa mkutano wa kuchagua mwakilishi wa mkoa huo katika Kamati ya Utekelezaji ya Taifa (KUT) ya chama hicho.

Shesha amesema hadi wakati huo, kikao kimoja tu cha mabaraza ya wafanyakazi kilikuwa kimefanyika, hali iliyomsukuma kuiomba Serikali ya Mkoa kuwakumbusha waajiri umuhimu wa kukamilisha vikao vinavyotakiwa.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuelekeza uwekezaji katika miradi mbalimbali ya sekta ya elimu, pamoja na maelekezo yake kuhusu ulipaji wa stahiki za walimu.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Richard Kayombo, ameahidi kushughulikia maombi yaliyowasilishwa na walimu, yakiwemo madai yao yanayohitaji ufumbuzi katika ngazi ya mkoa.

Kayombo pia amewataka walimu kujiandaa katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha mvua za El NiƱo haziathiri ratiba za masomo na shughuli nyingine za ufundishaji na ujifunzaji.

Vilevile, amewakumbusha walimu kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza umuhimu wa sekta ya elimu kwenda sambamba na taasisi nyingine katika kufanikisha malengo ya dira hiyo.

Katika uchaguzi huo, Mwita Magige, aliyechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya CWT Taifa, ameahidi kusimamia na kupigania haki na maslahi ya walimu, pamoja na kuwasilisha changamoto zao katika ngazi husika ili ziweze kufanyiwa kazi.

Magige amesema atatumia nafasi hiyo kuhakikisha hoja za walimu zinapata uwakilishi na kufikishwa kwa mamlaka zinazohusika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...