Na Said Mwishehe,Michuzi TV


MATUMIZI ya teknolojia za kidijitali pamoja na Akili Unde (AI)yanatarajiwa kuwa miongoni mwa nyenzo muhimu za kuboresha usimamizi na kuongeza ufanisi katika Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (SACCOS) Barani Afrika.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 14,2026 jijini Dar es Salaam na Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk.Benson Ndiege alipokuwa akizungumzia mijadala inayoendelea katika Kongamano la Kimataifa la vyama vyq akibq na mikopo barani Afrika linaloendelea nchini Tanzania.

“Matumizi ya teknolojia ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele cha juu katika Mkutano Mkuu wa 26 wa SACCO unaofanyika nchini Tanzania.Watalaam kutoka ndani na nje ya nchi wanajadili namna teknolojia inavyoweza kutumika kuongeza ufanisi katika shughuli za vyama vya ushirika na kuhamasisha wananchi kujiunga na taasisi hizo.”

Amefafanua majadiliano hayo yanalenga kupata mapendekezo na maazimio ya pamoja yatakayosaidia vyama vya ushirika kutumia teknolojia kukabiliana na changamoto za kiutendaji na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wanachama.

“Kupitia matumizi ya teknolojia kunawezesha kuboresha shughuli mbalimbali katika vyama vyetu vya ushirika.Kwa mfano kupitia teknolojia tunatunza kumbukumbu zetu na vigumu kumbukumbu hizo kupotea ukilinganisha na kutunza kumbukumbu katika katarasi.Hivyo teknolojia ni moja ya eneo ambalo limepewa kipaumbele kwa kuhakikisha tunaitumia vema katika kuendesha shughuli zetu.”

Pia amesema kongamano hilo linatoa fursa ya pekee kwa washiriki kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo ya kiteknolojia na namna yanavyoweza kutumika kuboresha utendaji wa vyama katika mazingira ya sasa ya kidijitali.

Mbali na teknolojia, Dk.Ndiege amesema matumizi ya mifumo ya kisasa yanajadiliwa sambamba na utawala bora, usimamizi wa vyama, matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi pamoja na kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake.

Amesisitiza matumizi sahihi ya takwimu ni nguzo muhimu katika kuimarisha maamuzi ya kiutendaji, huku mifumo bora ya usimamizi ikitarajiwa kusaidia kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika shughuli za kila siku za SACCOS.

Kwa mujibu wa Dk.Ndiege, vijana na wanawake ni miongoni mwa makundi makuu yanayolengwa katika mafunzo ya mkutano huo, kwa kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo endelevu ya sekta ya ushirika.

Ameeleza kwamba kuimarisha ushiriki wa makundi hayo, pamoja na kutumia teknolojia ipasavyo, kutaongeza fursa za wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma zinazotolewa na vyama hivyo.

Mkutano huo ulioanza Oktoba 11, 2026, unatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 16 mwaka hi ukiwa na programu mbalimbali za mafunzo, mijadala na ubadilishanaji wa uzoefu kuhusu usimamizi na maendeleo ya SACCOS.

Dk.Ndiege alibainisha kuwa kongamano hilo lililoshirikisha mataifa 28 pia ni fursa kwa Tanzania kujifunza kutoka kwa nchi nyingine kuhusu mbinu bora za kuboresha usimamizi wa vyama vya ushirika kupitia teknolojia.

Washiriki wa kongaamano hilo ni pamoja na viongozi wa sekta ya ushirika, mawaziri na makatibu wakuu kutoka nchi za Botswana, Uganda, Zambia, Kenya na mataifa mengine ya Afrika na nje ya bara hilo.

Akihitimisha, Dk.Ndiege amesema ingawa sekta ya ushirika iliwahi kukabiliwa na changamoto za usimamizi zilizotikisa imani ya wananchi, kuimarisha utawala bora na kutumia teknolojia kutasaidia kujenga imani hiyo upya na kuleta ufanisi wa muda mrefu.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...