Na Oscar Assenga, Tanga

MKUU mpya wa Wilaya ya Pangani, Mwanaidi Adadi Rajabu, ameahidi kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo pamoja na fursa mbalimbali zilizopo wilayani humo kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo.

Mwanaidi ametoa ahadi hiyo mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Pangani katika hafla iliyofanyika mkoani Tanga, akimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini vijana na kuwapa nafasi za uongozi katika taifa.

Alisema Pangani ina fursa nyingi za maendeleo na uwekezaji ambazo zinahitaji kusimamiwa kwa karibu ili ziweze kuwanufaisha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo.

“Katika wilaya ya Pangani kuna fursa nyingi sana ambazo tunakwenda kuzisimamia, ikiwemo miradi ya Serikali iliyopo na ambayo itaendelea kuletwa katika wilaya yetu,” alisema.

Mwanaidi pia alimpongeza Rais Samia kwa namna anavyoendelea kuiunga mkono Tanga, hususan Wilaya ya Pangani, kupitia utekelezaji wa miradi na uwekezaji mbalimbali wa maendeleo.

Alisema miongoni mwa fursa zilizopo Pangani ni Hifadhi ya Taifa ya Saadani, bahari, kilimo cha minazi pamoja na uwekezaji katika miundombinu, ikiwemo ujenzi wa daraja kubwa unaotekelezwa kwa uwekezaji wa Serikali.

“Maendeleo ni mengi Pangani na fursa za uwekezaji ni nyingi. Tunamshukuru Rais kwa kuendelea kutuona wana-Pangani na kuendelea kuleta maendeleo katika eneo letu,” alisema.

Akizungumzia namna atakavyowatumikia wananchi, Mwanaidi alisema atahakikisha anakuwa karibu nao kwa kuwafikia walipo na kusikiliza kero zinazowakabili, akieleza kuwa atatumia uzoefu alioupata katika uongozi wake wa awali wilayani Korogwe.

Alisema elimu ni miongoni mwa maeneo atakayoyapa kipaumbele, huku akieleza kuwa tayari wamejipanga kuboresha mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa madarasa na upatikanaji wa madawati.

Aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwa kuwa wao ndio taifa la kesho, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana katika kuboresha elimu kwa ajili ya maendeleo ya Pangani na taifa kwa ujumla.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...