-Asema hati ya kurasimisha hadhi ya Bagamoyo itapatikana wiki ijayo
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameelekeza wananchi wa maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo, lakini bado yana mazingira ya vijijini, waendelee kuunganishiwa umeme kwa gharama ya Sh. 27,000, akisisitiza kuwa mabadiliko ya hadhi hayamaanishi kuongezeka kwa uwezo wao wa kiuchumi.
Ametoa maelekezo hayo leo, Ijumaa, Oktoba 16, 2026, alipozungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja.
Amesema baadhi ya maeneo yanapotangazwa kuwa miji midogo, wananchi wake huchukuliwa kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha, ilhali hali zao za maisha bado ni za vijijini. Ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuzingatia hali hiyo katika kuwaunganishia huduma.
“Wananchi hawa wanaoitwa mji mdogo niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini,” amesema.
Kuhusu hadhi ya Bagamoyo, Dkt. Mwigulu amewahakikishia wananchi kuwa hati ya kuirasimisha itapatikana wiki ijayo, akisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya uamuzi na kinachobaki ni kukamilisha taratibu.
“Mheshimiwa Rais tayari alishakwisha kufanya uamuzi, na mimi niwahakikishie mwezi huu huu, wiki ijayo, mtakuwa mmeshapata hati hiyo,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwagiza Kamishna wa Ardhi kuongoza mwenyewe kliniki ya kusikiliza na kushughulikia kero za ardhi za wananchi wa Bagamoyo kuanzia Jumatatu ijayo. Ameelekeza afike na timu kutoka makao makuu, ikishirikiana na wataalamu wa mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kufanya kazi wiki nzima.
“Usitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesema migogoro ya ardhi inahatarisha undugu na mshikamano, na tayari amewaelekeza Waziri wa Ardhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri anayesimamia TAMISEMI kupitia upya utaratibu wa kuitatua. Aidha, amesisitiza wananchi wanaopisha uwekezaji na miradi ya maendeleo walipwe fidia stahiki bila kupunjwa.
Kuhusu huduma za afya, amekataza kuwachangisha wananchi fedha za mafuta ya magari ya kubebea wagonjwa wanaopelekwa hospitali za rufaa, akisisitiza kuwa mamlaka zinazoyasimamia zinapaswa kuhakikisha yana mafuta na yanatoa huduma iliyokusudiwa.
Pia, amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutokuzuia miili ya marehemu hospitalini kutokana na madai ya malipo. Amevielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kufuatilia ununuzi, usambazaji na matumizi ya dawa za serikali ili kuhakikisha zinawafikia wananchi.
Waziri Mkuu amesema sekta binafsi imara na viwanda vya kuchakata mazao ni muhimu katika kuongeza ajira na kipato. Amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji na uzalishaji, huku akisisitiza matumizi bora ya ardhi na uzingatiaji wa sheria.




















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...