Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemuagiza Kamishna wa Ardhi Tanzania, Nathaniel Mathew Nhonge, kufika Bagamoyo Oktoba 19, 2026, kuongoza kliniki maalumu ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo.
Dkt. Mwigulu amemtaka Kamishna huyo kufika mwenyewe akiwa na timu ya wataalamu kutoka makao makuu, kwa kushirikiana na wataalamu wa mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ili kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa muda wa wiki moja.
“Usitume mwakilishi, uje mwenyewe kusikiliza mtu mmoja mmoja wewe mwenyewe,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Amesema migogoro ya ardhi inahatarisha undugu na mshikamano katika jamii, hivyo amewaelekeza Waziri wa Ardhi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri anayesimamia TAMISEMI kupitia upya mifumo ya kushughulikia migogoro hiyo kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu.
Kuhusu wananchi wanaopisha maeneo kwa ajili ya uwekezaji na miradi ya maendeleo, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa wanapaswa kulipwa fidia stahiki bila kupunjwa, akieleza kuwa haki zao lazima zilindwe wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika hatua nyingine, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuendelea kuwaunganishia umeme kwa gharama ya Sh. 27,000 wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyopandishwa hadhi kuwa miji midogo, lakini ambayo bado yana mazingira yanayofanana na vijijini.
Amesema kupandishwa hadhi kwa maeneo hayo hakumaanishi kuwa wananchi wameongezewa uwezo wa kiuchumi, hivyo hawapaswi kunyimwa fursa ya kupata huduma ya umeme kwa gharama wanazoweza kumudu.
“Wananchi hawa wanaoitwa mji mdogo, niwaelekeze watu wa TANESCO, umeme waendelee kuunganishiwa kwa 27,000 ile ile ya kijijini,” amesema.
Kuhusu urasimishaji wa makazi Bagamoyo, Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi kuwa hati ya urasimishaji inatarajiwa kupatikana wiki ijayo, akieleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amefanya uamuzi na kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu zilizobaki.
Dkt. Mwigulu ametoa maagizo hayo Oktoba 16, 2026, wakati akizungumza na wananchi mjini Bagamoyo, mkoani Pwani, katika ziara yake ya kikazi ya siku moja




















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...