Na Byera Deus, Bukoba

WIZARA ya Afya imeitambulisha rasmi taasisi ya kimataifa ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF) kuwa mdau mpya wa kuratibu na kuendeleza afua za VVU na UKIMWI mkoani Kagera na mikoa mingine sita nchini, kufuatia kukamilika kwa shughuli za uratibu zilizokuwa zikitekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Management and Development for Health (MDH) tangu Septemba 2026.

MDH imetekeleza shughuli hizo kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kipindi cha miaka 13, huku ujio wa EGPAF ukilenga kuendeleza juhudi za kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na virusi hivyo.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa taasisi hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa EGPAF, Dkt. Sajida Kimambo, alisema taasisi hiyo inalenga kuchangia kufikiwa kwa malengo ya kimataifa ya 95-95-95 ifikapo mwaka 2030, yanayolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao, asilimia 95 ya waliotambua hali zao wanapata matibabu na asilimia 95 ya wanaopata matibabu wanafikia kiwango cha kufubaza virusi.

Alisema moja ya maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wa mradi huo ni kuimarisha huduma kwa wanawake wajawazito ili kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.

Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha watoto wanazaliwa na kukua bila kuambukizwa VVU kutoka kwa mama zao, hivyo kulinda afya zao na kupunguza maambukizi mapya katika jamii.

Aidha, alisema mradi huo utajikita katika kuwafikia vijana balehe kwa kuimarisha elimu, uelewa na upatikanaji wa huduma za kinga, upimaji na matibabu ya VVU na UKIMWI.

Dkt. Kimambo alibainisha kuwa mabadiliko muhimu katika utekelezaji wa mradi huo ni matumizi ya mfumo wa ufadhili unaozingatia matokeo, ambapo utoaji wa fedha za wafadhili utahusishwa na matokeo yaliyofikiwa.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bwai Biseko, alisema mkoa huo uko tayari kushirikiana na EGPAF katika kuendeleza afua za VVU na UKIMWI ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata huduma zinazohitajika.

Hata hivyo, aliiomba taasisi hiyo pamoja na wafadhili kuzingatia vijana waliokuwa wamepata mafunzo na kushiriki katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa kupitia miradi iliyokuwa ikitekelezwa na MDH.

Alisema baadhi ya vijana hao wamekata tamaa baada ya shughuli za MDH kumalizika, hivyo kusisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi ya kuendelea kutumia ujuzi na uzoefu walioupata katika sekta ya afya.

Naye Mshauri wa Programu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Anath Rwebembela, alisema mradi huo unatarajiwa kufadhiliwa na Serikali ya Marekani kwa kipindi cha mwaka mmoja, hatua itakayowezesha kutathmini utekelezaji wake na matokeo yatakayopatikana kabla ya kuangalia uwezekano wa kuongeza muda wa mkataba ili kuendelea na afua hizo hadi mwaka 2030.

Alisema EGPAF imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya nchini kwa muda mrefu, hivyo ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha juhudi za kuzuia maambukizi mapya ya VVU, kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na virusi hivyo na kuwalinda watoto pamoja na vijana dhidi ya maambukizi.

Utambulisho wa EGPAF uliwakutanisha wakurugenzi wa halmashauri, waganga wakuu wa halmashauri, waganga wafawidhi wa vituo vya afya, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu majukumu ya mdau huyo mpya na mwelekeo wa utekelezaji wa mradi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...