Na Mwandishi Wetu, Pretoria – Afrika Kusini
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Nchi Tatu (TPC) za Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini, uliojadili mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka.
Mkutano huo umefanyika Oktoba 15, 2026, jijini Pretoria, Afrika Kusini, baada ya kikao cha viongozi waandamizi kufanyika Oktoba 14, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Kabudi amezitaka nchi wanachama kuimarisha ushirikiano kwa kubadilishana taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini wahalifu, kuvunja mitandao yao na kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka.
Amesema mkutano huo ulilenga kujadili mikakati ya kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya katika ukanda wa Bahari ya Hindi pamoja na uhalifu mwingine, ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu, utekaji nyara na uhalifu wa kuvuka mipaka.
Profesa Kabudi amesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya vyombo vya usalama ni muhimu katika kudhibiti vitendo vya uhalifu vinavyotumia mianya ya mipaka na udhaifu wa mifumo ya udhibiti kutekeleza shughuli haramu.
Katika hatua nyingine, amewakaribisha rasmi wanachama wa TPC nchini Tanzania, ambayo kwa kushirikiana na Kenya na Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika Juni na Julai 2027.
Amesisitiza umuhimu wa nchi hizo kutumia fursa ya mashindano hayo kuimarisha mikakati ya kupambana na dawa za kulevya na uhalifu mwingine, akieleza kuwa matukio makubwa ya kimataifa yanaweza kutumiwa na wahalifu kutekeleza shughuli zao haramu.
Aidha, mkutano huo umeridhia maombi ya Angola na Uganda kujiunga na TPC, ambayo makao yake makuu yako nchini Msumbiji.
Kwa hatua hiyo, ushirikiano huo sasa unahusisha nchi tano ambazo ni Afrika Kusini, Angola, Msumbiji, Tanzania na Uganda, hatua inayolenga kupanua wigo wa ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka.
Mkutano huo uliwakutanisha pia viongozi waandamizi kutoka mamlaka za kudhibiti dawa za kulevya, vyombo vya polisi na wadau wa maendeleo, wakiwemo Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) pamoja na Umoja wa Ulaya.
Washiriki kutoka Angola, Uganda, Comoro, Shelisheli, Eswatini, Uingereza na Marekani nao walishiriki majadiliano kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto za uhalifu, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...