Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro

NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuboresha miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano, pamoja na kuimarisha vitendea kazi na kutoa elimu kwa watumishi na wadau ili kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño zinazotarajiwa.

Akiwa katika ukaguzi wa miundombinu ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mabula ameelekeza kasi ya maboresho iongezwe katika maeneo hatarishi, maandalizi ya mitambo na huduma za afya, pamoja na kutolewa kwa mafunzo ya vitendo kwa timu za uokoaji zinazojumuisha maafisa na askari wa uhifadhi.

“Kama El Niño itakuja, itukute tumejiandaa. Mitambo, magari ya huduma, mafuta na vipuri viwepo wakati wote ili kuhakikisha usalama wa watalii, wananchi na rasilimali za wanyamapori na malikale zilizopo,” amesema Mabula.

Ameongeza kuwa ni muhimu kuweka alama katika maeneo hatarishi ili kuongeza tahadhari kwa watumiaji wa barabara na maeneo mengine yanayoweza kuathiriwa na mvua hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro, SACC Gloria Bideberi, amesema mamlaka hiyo imeendelea kutoa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na athari za mvua hizo kwa makundi mbalimbali.

Amesema hadi sasa elimu imetolewa kwa watumishi 200, viongozi wa vijiji na kata 275, wanafunzi zaidi ya 1,550 na wananchi 4,965 katika kata 10 zilizopo ndani ya hifadhi.

Aidha, amesema maeneo 80 ya huduma za malazi yamehusishwa katika maandalizi hayo, huku magari ya huduma za dharura na vifaa tiba vikiandaliwa kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shughuli za Miundombinu, Mhandisi Shaban Felician, amesema mitambo zaidi ya 11 imeandaliwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, pamoja na uokoaji wa magari ya wageni yanayoweza kukwama kutokana na mvua.

Amesema mamlaka hiyo pia inaendelea kuhakikisha mtandao wa barabara wenye urefu wa zaidi ya kilomita 600 ndani ya hifadhi unabaki kupitika katika msimu wote wa mvua, ili kuwezesha shughuli za uhifadhi na utalii kuendelea bila kukwama.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...