Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Serikali inatarajia kuzindua rasmi majengo 37 ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na kilomita 57.1 za barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utendaji wa Serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Palamagamba Kabudi, amesema majengo yatakayozinduliwa yanajumuisha majengo 24 ya wizara na 13 ya taasisi za Serikali. Ameeleza kuwa ujenzi wa barabara hizo za lami umegharimu Shilingi Bilioni 110.5.

Profesa Kabudi amesema kukusanywa kwa wizara na taasisi za Serikali katika eneo moja kutarahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, kuboresha mawasiliano baina ya taasisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi. Hatua hiyo pia inalenga kupunguza changamoto zinazotokana na ofisi za Serikali kutawanyika katika maeneo mbalimbali.

Ameeleza kuwa majengo hayo ni sehemu ya awamu ya pili ya mradi wa Mji wa Serikali Mtumba, unaohusisha pia majengo mengine 35 ya taasisi mbalimbali yaliyokamilika nje ya eneo la Mji wa Serikali, yakiwemo yaliyopo Chang’ombe na Njedengwa.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, uwekezaji huo unaendelea kuimarisha hadhi ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na kitovu cha shughuli za Serikali, huku ukifungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi na sekta binafsi.

Amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa jiji la Dodoma, hususan katika sekta za usafirishaji, malazi, biashara na huduma za kitaalamu. Amesema kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kunatarajiwa kuongeza zaidi fursa hizo kadiri idadi ya watu wanaotembelea jiji hilo itakavyoongezeka.

Aidha, amewataka watumishi wa umma watakaofanya kazi katika Mji wa Serikali Mtumba kutumia miundombinu hiyo kwa ufanisi na kuzingatia misingi ya uwajibikaji, uadilifu, nidhamu na uzalendo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi amewaalika wananchi, hususan wakazi wa Dodoma, kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo. Amesema shamrashamra za kuelekea uzinduzi zitahusisha upigaji fataki usiku wa kuamkia Oktoba 30, 2026.

Amesisitiza kuwa mradi huo unaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendeleza miundombinu ya kisasa na kuimarisha utoaji wa huduma za umma nchini.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...