DENIS MLOWE, IRINGA

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewatangazia wananchi kuhusu ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, inayotarajiwa kufanyika mkoani humo Oktoba 18, 2026, ambapo atakagua miradi ya maendeleo ya elimu ya juu na miundombinu ya usafiri wa anga.

Akizungumza na waandishi wa habari, James alisema Makamu wa Rais atatembelea Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), ambako atakagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi saba yenye thamani ya Sh bilioni 30.4.

Alisema miongoni mwa miradi hiyo ni Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wenye thamani ya Sh bilioni 14.8, ujenzi wa maabara ya Fizikia na hosteli ya wanafunzi unaogharimu Sh bilioni saba, pamoja na ujenzi wa jengo la Sayansi na jengo la Midia Anuwai na Elimu Maalum unaogharimu Sh bilioni 7.8.

James alisema miradi hiyo inalenga kuboresha miundombinu ya elimu ya juu na mazingira ya kufundishia na kujifunzia, hatua itakayochangia kuimarisha utoaji wa elimu na kukuza maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, Makamu wa Rais atatembelea Uwanja wa Ndege wa Iringa uliopo Nduli kukagua ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari, mradi wenye thamani ya Sh bilioni 41.06.

Kheri James alisema uwekezaji huo unalenga kuboresha huduma za usafiri wa anga na kuongeza fursa za biashara na shughuli za kiuchumi mkoani Iringa.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Manispaa ya Iringa na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki katika shughuli za ziara hiyo, akieleza kuwa ni nafasi ya kushuhudia maendeleo ya miradi inayotekelezwa mkoani humo.

Rc James aliongeza kuwa Makamu wa Rais anatarajiwa kufika Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa saa 2:00 asubuhi na baadaye kutembelea Uwanja wa Ndege wa Nduli kwa ajili ya kukagua mradi wa jengo la abiria na maegesho ya magari.

James alisema wananchi wanatarajiwa kushiriki katika mapokezi na shughuli zitakazofanyika katika maeneo hayo, huku Makamu wa Rais akitarajiwa pia kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Iringa.

Kwa ujumla miradi saba ya MUCE ina thamani ya Sh bilioni 30.4, huku mradi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli ukiwa na thamani ya Sh bilioni 41.06, hivyo kufanya jumla ya uwekezaji katika miradi hiyo kuwa Sh bilioni 71.46.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...