Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imesema chanzo cha maji cha Makutupora kina mchango mkubwa katika upatikanaji wa huduma ya maji jijini Dodoma, kikizalisha zaidi ya nusu ya maji yote yanayozalishwa na mamlaka hiyo kwa siku.

Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 26, 2026, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph, amesema chanzo hicho ni nguzo muhimu katika kukidhi mahitaji ya maji kwa wakazi wa jiji hilo, kutokana na uwezo wake mkubwa wa uzalishaji ikilinganishwa na vyanzo vingine vinavyotumiwa na mamlaka hiyo.

Amesema kwa sasa mahitaji ya maji jijini Dodoma yanafikia lita milioni 159.9 kwa siku, huku DUWASA ikiwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 91 pekee kwa siku, hali inayoonesha kuwepo kwa pengo kubwa kati ya mahitaji ya wananchi na maji yanayopatikana.

Mhandisi Joseph amesema chanzo cha Makutupora huzalisha lita milioni 61.5 kwa siku, huku kiasi kingine cha maji kikitokana na vyanzo mbalimbali vidogo vilivyosambaa katika maeneo tofauti ya jiji, ikiwemo Nzuguni, Iyumbu, Nala, Ihumwa, Nkuhungu, Miganga, Mkonze na Makulu.

Ameeleza kuwa licha ya mchango wa vyanzo hivyo, upatikanaji wa maji bado unaathiriwa na uhaba wa vyanzo vya uzalishaji. Kwa sasa, DUWASA ina visima 72 vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali, vikiwemo visima 17 vilivyopo Makutupora ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa maji jijini humo.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mhandisi Joseph amesema mamlaka hiyo imeweka mpango wa miaka mitano unaolenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 91 hadi lita milioni 121 kwa siku, hatua inayotarajiwa kupunguza pengo kati ya maji yanayozalishwa na mahitaji ya wananchi.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Dodoma, sambamba na kukabiliana na ongezeko la mahitaji linalotokana na kukua kwa jiji na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa huduma hiyo.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...