Na Mwandishi Wetu, Mirerani

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, wameilalamikia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu migodi mingi ya madini ya Tanzanite kutotekeleza ipasavyo miradi ya Uwajibikaji kwa Kampuni kwa Jamii (CSR) na kulipa tozo za huduma kwa jamii (Service Levy).

Wametoa malalamiko hayo mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Subira Mgalu, ilipotembelea machimbo ya madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kaleiya Melita Mollel, amesema wamiliki wengi wa migodi ya Tanzanite hawachangii ipasavyo maendeleo ya jamii kupitia CSR na tozo za huduma, licha ya wajibu huo kuwepo kisheria.

Amesema ni kampuni chache tu zinazoshiriki katika shughuli hizo, akizitaja Franone, Chusa Mining, God Charity na kampuni zinazohusishwa na bilionea Laizer kuwa miongoni mwa zinazochangia maendeleo ya jamii.

“Ni kampuni chache zinazotekeleza CSR au kulipa Service Levy, jambo ambalo lipo kisheria, lakini kampuni nyingi zimekuwa zikisuasua,” amesema Mollel.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji ya Halmashauri hiyo, Albert Msole, amesema kampuni nyingi za uchimbaji hazina mwitikio wa kutosha katika kuchangia maendeleo ya halmashauri, licha ya suala hilo kuwa na msingi wa kisheria.

Amesema halmashauri imekuwa ikibeba mzigo wa kulea na kusomesha baadhi ya watoto yatima ambao wazazi wao walifariki dunia baada ya kuugua magonjwa ya kifua yaliyohusishwa na mazingira ya kazi migodini.

“Suala la kampuni za uchimbaji kuchangia CSR limekuwa likichukuliwa kama hisani, japokuwa lipo kisheria. Ni kampuni chache tu zilizotajwa na mwenyekiti ndizo zinazochangia,” amesema Msole.

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Madini, Steven Lemomo Kiruswa, amesema kampuni za uchimbaji zinapaswa kuzingatia wajibu wa kuchangia miradi ya CSR kwa mujibu wa sheria.

Amesema hata katika Mkoa wa Geita, ambako utekelezaji wa CSR unaonekana kufanya vizuri, bado wabunge wamekuwa wakilalamikia kiwango cha fedha zinazotolewa, wakitaka kiongezwe.

“Hata kule Geita, ambako CSR inafanya vizuri, bado wabunge wanalalamikia kiwango kinachotolewa kuwa ni kidogo, hivyo kinapaswa kuongezwa,” amesema Kiruswa.

Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdurahman Mwanga, amesema utekelezaji wa CSR ni wajibu wa kisheria kwa kampuni za uchimbaji, akibainisha kuwa suala hilo limeainishwa katika Kifungu cha 105 cha sheria husika.

Amesema halmashauri zinapaswa kuweka mwongozo utakaosaidia kusimamia utekelezaji wa wajibu huo na kuhakikisha jamii zinazozunguka migodi zinanufaika na shughuli za uchimbaji.

Kuhusu tozo ya huduma kwa jamii (Service Levy), Dkt. Mwanga amesema kampuni zinapaswa kulipa kwa mujibu wa masharti ya sheria, akitaja kiwango cha asilimia 0.3 ya mauzo ghafi kwa mwaka kwa kampuni zinazohusika katika eneo la Simanjiro.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...