Na Byera Deus, Karagwe
UJENZI wa Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Rwakajunju, wilayani Karagwe, mkoani Kagera, umefikia asilimia 79 ya utekelezaji wake, huku ukitarajiwa kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi mwishoni mwa Desemba 2026.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa mkombozi kwa wananchi zaidi ya 350,000 wa wilaya hiyo kwa kuboresha upatikanaji wa maji na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Kundo alisema upatikanaji wa maji utawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi, huku sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda, zikitarajiwa kunufaika kwa kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa eneo hilo.
Alisema mradi huo unaogharimu zaidi ya Sh bilioni 63 umeanza kuonesha matumaini kwa wananchi ambao wamekuwa wakisubiri huduma hiyo kwa muda mrefu.
“Nimepata maelezo kutoka kwa wasimamizi kuhusu kazi zilizokamilika na zinazoendelea kutekelezwa, na nimejionea maendeleo yaliyofikiwa. Ziara nyingi zilizopita tuliondoka tukiwa na hali isiyoridhisha, lakini leo matumaini ya wananchi kupata maji yameanza kuonekana,” alisema Kundo.
Alisisitiza kuwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo anapaswa kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa ili wananchi wa Omurushaka waanze kupata huduma ya maji safi na salama ifikapo mwishoni mwa Desemba mwaka huu.
Aidha, amemtaka msimamizi wa Mamlaka ya Bonde kuhakikisha chanzo cha maji kinachotumika katika mradi huo kinalindwa dhidi ya shughuli zinazoweza kusababisha uharibifu wa mazingira na kuhatarisha upatikanaji wa maji kwa siku zijazo.
Alisema utunzaji wa chanzo cha maji ni muhimu katika kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na unaendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo, Evodius Byeyanga, alisema kazi mbalimbali zinaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha mradi unakamilika, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya chanzo cha maji na utandazaji wa mabomba kuelekea mji wa Omurushaka.
Byeyanga alisema Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Rwakajunju ulianza kutekelezwa Aprili 2023 na awali ulitarajiwa kukamilika Desemba 2025. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji, mkandarasi aliongezewa muda hadi Julai 2027.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kupunguza adha ya wananchi kutafuta maji na kuboresha mazingira ya ukuaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Karagwe na maeneo mengine yatakayohudumiwa.
Aliongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji katika miji ya Kayanga na Omurushaka kutoka asilimia 65 hadi asilimia 100.



.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...